Vardy aanza na bao, Atletico mambo magumu
Muktasari:
- Sare hii inaonyesha kuwa Leicester City inaweza kufanya vizuri kwenye msimu huu wa Ligi Kuu England kutokana na kiwango ambacho wamekionyesha.
London, England. Jamier Vardy ameendeleza moto wake baada ya Leicester City kupanda daraja na kuifungia timu yake bao ililoipa timu yake sare ya 1-1 dhidi ya Tottenham, huku Atletico Madrid wakibanwa kwenye La Liga.
Vardy (37) alifunga bao la kusawazisha kwa kikosi hicho katika dakika ya 57 kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England kwao tangu waliposhuka daraja baada ya awali beki Pedro Porro kuifungia Spurs.
Sare hii inaonyesha kuwa Leicester City inaweza kufanya vizuri kwenye msimu huu wa Ligi Kuu England kutokana na kiwango ambacho wamekionyesha.
Hata hivyo, kipindi cha pili cha mchezo huo, timu hiyo ndiyo ilionekana kuchakarika zaidi huku ikipoteza nafasi kadhaa za wazi.
"Tunajaribu kupambana kuhakikisha kuwa tunapata pointi muhimu kwenye kila mchezo, hii ilikuwa mechi yetu muhimu na tunashukuru kwa pointi moja ambayo tumeipata, tunaona ni mwanzo mzuri na mashabiki wetu ambao walishuka daraja nasi wamefurahi," amesema Vardy.
Hii ni sare ya nne kwenye michezo ya kwanza ya ligi hiyo, ambapo timu nane zimefanikiwa kushinda na nane zimepoteza.
La Liga
Kwenye Ligi Kuu ya Hispania La Lig,a usiku wa kuamkia leo pia ulipigwa mchezo mmoja ambapo vijana wa kocha Diego Simeone, Atletico Madrid, walifanikiwa kuambulia sare ya mabao 2-2 dhidi ya Villarreal kwenye mchezo mkali na wa kuvutia.
Arnaut Danjuma alifanikiwa kuifungia Villarreal katika dakika ya 18 tu ya mchezo huo, Marcos Llorente akasawazisha katika dakika ya 20, huku Koke akijifunga dakika ya 37 na kuipa uongozi Villarreal lakini Atletico ikafunga la pili katika dakika ya 45 kupitia kwa Alexander Sorloth na kuifanya mchezo hiyo kumalizika kwa sare.
Katika ligi hiyo, ambayo ilianza Ijumaa iliyopita ni timu nne tu zimefanikiwa kuibuka na ushindi kwenye michezo yao ya kwanza ya ligi ambazo ni Celta Vigo wanaoongoza ligi, Barcelona, Roya Vallecano na Real Valladolid.