Van Dijk atuliza joto Liverpool

Muktasari:
- Straika Darwin Nunez na Curtis Jones walishuhudia mikwaju yao ya penalti ikiokolewa na kipa Gianluigi Donnarumma kwenye mchezo wa marudiano wa hatua ya mtoano uwanjani Anfield na hivyo kuiruhusu Paris Saint-Germain kusonga mbele na kutinga robo fainali.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk amemtaka straika Darwin Nunez na wachezaji wenzake wa kikosi hicho cha Anfield wasikate tamaa baada ya kutupwa nje ya mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Jumanne iliyopita.
Straika Darwin Nunez na Curtis Jones walishuhudia mikwaju yao ya penalti ikiokolewa na kipa Gianluigi Donnarumma kwenye mchezo wa marudiano wa hatua ya mtoano uwanjani Anfield na hivyo kuiruhusu Paris Saint-Germain kusonga mbele na kutinga robo fainali.
Bao la Ousmane Dembele la dakika za mapema liliifanya miamba hiyo ya Ufaransa kuongoza 1-0 na kufanya ubao wa matokeo wa jumla kuchomeka 1-1 baada ya Liverpool nayo kushinda 1-0 kwenye mechi ya kwanza. Lakini, Van Dijk anataka wachezaji wenzake wa Liverpool kuhamishia nguvu kwenye michuano mingine ili kufikia malengo yao ya msimu huu.
Taji la kwanza kwa kocha Arne Slot kwenye kikosi hicho cha Liverpool linaweza kupatikana endapo kama watafanikiwa kuichapa Newcastle United kwenye fainali ya Kombe la Ligi. Na kwenye hilo, nahodha huyo wa Liverpool, Van Dijk anataka wajiweke sawa kabla ya kufikia wikiendi ili kwenda Wembley kushinda na kufuta kumbukumbu zote mbaya za kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa.
"Soka ndivyo lilivyo," alisema Van Dijk baada ya mechi na kuongeza. "Niliwaambia vijana 'msihuzunike kwasababu tumetolewa kwenye michuano, bali tuwe vifua mbele'. Sasa tujiandaa kwa changamoto mpya ya wikiendi ambayo ni nzuri zaidi.
"Nadhani tulikuwa vizuri na tungeweza kufika mbali, lakini tulifahamu baada ya kupangwa na PSG itakuwa ngumu. Tuliona tulivyotaabika Paris, lakini tukashinda na hapa tumeona jinsi Liverpool ilivyokuwa timu nzuri, lakini tumeshatupwa nje ya michuano."
Kocha wa PSG, Luis Enrique amesifu kiwango cha Liverpool, lakini amemsifia zaidi kipa wake, Donnarumma, aliposema: "Timu zote zilistahili kusonga mbele. Walicheza vizuri zaidi yetu, lakini nadhani timu yangu hapa Anfield imeonyesha kile inachoweza kukifanya. Tulijaribu kucheza kwenye ubora wetu, lakini ilikuwa ngumu kwa sababu walikuwa hatari sana. Timu zote zilistahili kufuzu. Tulikuwa na bahati, wamegongesha mwamba mara kadhaa. Gigi (Gianluigi Donnarumma) alikuwa kama Alisson kwenye mechi ya kwanza. Tumefurahi kutinga raundi inayofuata."