Uzi mpya wa Man United Sh250,000

Muktasari:
- Makinda wa klabu hiyo Kobbie Mainoo, Alejandro Garnacho na Rasmus Hojlund - wenye umri wa miaka 19, 20, na 21 mtawalia, walitangaza jezi hizo kwa staili yao maarufu ya kushangilia ambayo walikaa kwenye bango la matangazo ya uwanjani.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imetambulisha jezi mpya ya nyumbani watakayovaa nyota wake kwenye Ligi Kuu England msimu wa 2024/2025 huku wakiwa na matarajio makubwa chini ya kocha wao Mdachi, Erik Ten Hag.
Makinda wa klabu hiyo Kobbie Mainoo, Alejandro Garnacho na Rasmus Hojlund - wenye umri wa miaka 19, 20, na 21 mtawalia, walitangaza jezi hizo kwa staili yao maarufu ya kushangilia ambayo walikaa kwenye bango la matangazo ya uwanjani.
Picha hiyo ni kitu ambacho mashabiki wa Man United watapenda kuona kinatokea muda wote. Staili hiyo ya kushangilia, ilitokea wakati Garnacho alipofunga bao kwenye ushindi wa mabao 3-0 iliyopata Man United nyumbani, ambapo kwenye kushangilia aliungana na makinda wenzake, Mainoo na Hojlund waliokwenda kukaa kwenye mabango ya matangazo ya uwanjani Old Trafford.
Wachezaji hao watatu waliweka mikono yao kwenye mabega ya kila mmoja na kufanya picha hiyo kuwa maarufu sana mitandaoni, hivyo waliamua kurudia tukio hilo wakati wanatangaza uzi wao mpya utakaotumika kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.
Makinda hao watatu ndiyo wachezaji pekee wenye uhakika wa kubaki kwenye kikosi cha Man United, hakuna ambaye atauzwa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Hapo mwanzoni kwenye orodha ya wachezaji wasioguswa huko Old Trafford kulikuwapo pia na jina la Andre Onana, lakini kwa sasa chochote kinaweza kutokea kwa kipa huyo wa kimataifa wa Cameroon.
Jezi hiyo nyekundu yenye michirizi myeupe na bukta nyeupe imepambwa na mdhamini mkuu mpya wa kwenye jezi, Snapdragon. Jezi hiyo imetengenezwa kwa kuzingatia jezi zilizowahi kuvaliwa na timu hiyo katika kipindi cha Busby Babes mwaka 1952.