Prime
Gwiji kasema! Gyokeres ni wa Man United tu

Muktasari:
- Man United kwa muda mrefu imekuwa ikifukuzia huduma ya mchezaji huyo kutoka Sporting Lisbon.
LONDON, ENGLAND: STRAIKA gwiji, Alan Shearer anaamini Viktor Gyokeres atasaini kuichezea Manchester United licha ya sakata lake la usajili kuonekana kuwa gumu.
Man United kwa muda mrefu imekuwa ikifukuzia huduma ya mchezaji huyo kutoka Sporting Lisbon.
Staa huyo amekuwa kwenye rada za Man United baada ya kuonyesha kiwango bora cha kufunga msimu uliopita. Kitendo cha mshambuliaji huyo kuhusishwa na Man United imezidi baada ya miamba hiyo ya Old Trafford kunolewa na kocha wa zamani wa Sporting, Ruben Amorim - ambaye ndiye aliyemfanya kuwa straika huyo matata kabisa.
Wapinzani wa Man United kwenye Ligi Kuu England, Arsenal nayo inahitaji saini ya straika huyo na Kocha Mikel Arteta anahitaji huduma ya straika mpya ili kuwa na kikosi cha kibabe msimu ujao.
Akizungumzia vita hiyo ya vigogo wawili kwenye kusaka saini ya Gyokeres, straika kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu England, Shearer anaamini Man United ndiyo itakayoibuka na ushindi kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya mshambuliaji huyo na kjocha Amorim.
Akizungumza juu ya hilo, Shearer alisema:
“Imemsajili Matheus Cunha na tutakwenda kuona mapinduzi mengine makubwa Man United miezi miwili ijayo. Wataondoa wachezaji wengi kwenye kikosi, hivyo watahitaji wachezaji wengine kuja ili kuifanya timu kuwa tofauti.
“Mambo yalikuwa mabaya kwa muda mrefu, lakini kila kitu kitakuwa sawa kwenye ubora huo huo wa Man United hii ya msimu huu. Pre-season kubwa itakuja kwenye timu hiyo na kila kitu kitakuwa sawa.
“Usajili wa Bryan Mbeumo bado haujakamilika na nafahamu kuna timu nyingine zinamtaka ikiwamo Newcastle. Spurs wanaweza kujaribu kuvamia dili hilo kwa kuwa na Kocha Thomas Frank, ambaye anaweza kuwa tatizo.
“Kuhusu Viktor Gyokeres, sitashangaa kama watampata kwa sababu alifanya kazi zuri sana huko Sporting akiwa na Ruben Amorim, hii kitu ina umuhimu wake.
“Man United haitacheza Ulaya mwaka huu, hawapo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hivyo watalazimika kulipa mishahara mikubwa ili kupata wachezaji inaowataka kwa sababu kuna timu nyingine zinawataka pia.”
Hivi karibuni ilidaiwa kwamba Gyokeres ameikataa Man United na kuchagua kwenda Arsenal, lakini mwenyewe aliandika kwenye Instagram Story, aliposema: “Kuna vitu vingi sana vinazungumzwa kwa sasa, vingi ni uongo. Nitazungumza wakati mwafaka utakapofika.”