Utamu wa EPL umerudi tena

Muktasari:
- Hata hivyo, utepe wa ligi hiyo utakatwa Ijumaa, Agosti 16 huko uwanjani Old Trafford, wakati Manchester United itakapokuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na Fulham, ambapo utakuwa mchezo wa kwanza wa ligi ya msimu wa 2024-25.
LONDON, ENGLAND: KUMEKUCHA. Utamu wa mikikimikiki ya Ligi Kuu England unarudi tena baada ya ratiba ya msimu wa 2024-25 kuwekwa hadharani, huku mabingwa watetezi Manchester City wakiwa na kibarua cha kuanzia ugenini Stamford Bridge kukabiliana na Chelsea, Agosti 18.
Hata hivyo, utepe wa ligi hiyo utakatwa Ijumaa, Agosti 16 huko uwanjani Old Trafford, wakati Manchester United itakapokuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na Fulham, ambapo utakuwa mchezo wa kwanza wa ligi ya msimu wa 2024-25.
Kocha wa Man United, Erik ten Hag ana matumaini kwamba kikosi chake kitacheza kwa kiwango bora katika mchezo huo dhidi ya The Cottagers, ili isijirudie ya Februari mwaka huu, ambapo miamba hiyo ya Old Trafford ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa vijana hao wa kocha Marco Silva.
Wikiendi ya kwanza tu kwenye Ligi Kuu England inaanza kwa moto mkali, ambapo huko Stamford Bridge, kocha Kieran McKenna, akianza kibarua chake kwenye ligi akiwa na chama la The Blues, atakuwa na mtihani wa kumkabili bosi wake wa zamani, Pep Guardiola na kikosi cha Man City.
Arsenal na kampeni yao ya kujaribu kunasa taji la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 20, safari hii safari itaanzia Emirates, ambapo watakipiga na Wolves, Jumamosi, Agosti 17.
Mechi nyingine matata kabisa kwenye wikiendi ya kwanza, itashuhudia timu iliyopanda daraja msimu huu, Ipswich Town itakayokuwa nyumbani Portman Road kukipiga na Liverpool, ambayo itakuwa chini ya kocha mpya, Arne Slot baada ya Jurgen Klopp kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kudumu na miamba hiyo ya Anfield kwa miaka tisa.
Msimu uliomalizika, Man City ilihitaji ushindi kwenye mchezo wao wa mwisho dhidi ya West Ham United na kufanikiwa kuipiku Arsenal kwenye vita hiyo ya ubingwa wa ligi hiyo. Kwa upande mwingine wa msimamo, kulikuwa na timu tatu Luton, Burnley na Sheffield United zilishuka daraja na kwamba msimu ujao zitacheza kwenye Championship.
Kwa maana hiyo, kutakuwa na sura mpya kwenye ligi, licha ya kwamba mbili zilishuka daraja mwaka jana, ambazo ni Leicester City na Southampton, zilizorejea kwenye ligi, huku wapya ambao hawakuonekana kwenye Ligi Kuu England kwa zaidi ya miaka 20 ni Ipswich Town.
Msimu wa 2024-25 hakutakuwa na mapumziko ya kupisha kipindi cha baridi kwenye Ligi Kuu England, hivyo wachezaji watapewa muda zaidi wa kumpumzika hasa kwa wale ambao watatoka kwenye fainali za Euro 2024.
Msimu wa 2024-25 utahusisha wikiendi 33 pamoja na mechi za katikati ya wiki kwa wiki nne. Mechi za Boxing Day zitaendelea kuwapo kama ilivyo kwenye utamaduni wa Ligi Kuu England, licha ya mwaka msimu mpya hautakuwa na mechi za Mkesha wa Krismasi kama ilivyokuwa kwenye msimu wa 2023-24. Mechi tamu za kipindi cha sikukuu, zinahusisha pia kipute cha London Derby kati ya Chelsea na Fulham, wakati Arsenal yenyewe itakipiga na Ipswich huko Emirates.
Kama ilivyokawaida, mashabiki wa Ligi Kuu England watapata fursa ya kutazama mechi za mahasimu, ambapo kipute cha Merseyside Derby kinachokutanisha Liverpool na Everton kitapigwa Goodison Park, Desemba mwaka huu na marudiano itakuwa Anfield, Aprili mwakani.
Tottenham na Arsenal zitakutana Septemba mwaka huu kwenye mchezo wa kwanza, wakati ule wa marudiano utapigwa Januari huko Emirates, huku Manchester Derby ya kwanza itapigwa Etihad, Desemba na ile ya Old Trafford itapigwa Aprili.
Kwenye wikiendi ya kwanza. Everton, Newcastle United, Nottingham Forest na West Ham zitakipiga na Brighton, Southampton, Bournemouth na Aston Villa mtawalia.
Newcastle, Forest, Southampton, Tottenham na Wolves zitamaliza msimu kwa kucheza na Everton, Chelsea, Arsenal, Brighton na Brentford mtawalia, huku ligi hiyo ikitarajia kudhuhudia mechi 380.