Ulaya pamotoo! Juve na Inter, Barca, Madrid Bayern mzigoni
Muktasari:
- Huko Hispania, Jumamosi mikikimikiki ya La Liga itashuhudia Getafe ikishuka uwanjani kukipiga na Real Oviedo, wakati Real Madrid itakuwa ugenini kukipiga na Real Sociedad, huku Athletic Bilbao ikiwa na kazi mbele ya Alaves na Atletico Madrid itacheza na Villarreal.
MADRID, HISPANIA: MAPUMZIKO ya mechi za kimataifa yamekwisha na sasa shughuli imerejea kwenye Ligi Kuu za Ulaya na vikosi vya ligi bora vya huko Hispania, Ujerumani, Italia na Ufaransa vitaingia uwanjani kuonyeshana kazi.
Huko Hispania, Jumamosi mikikimikiki ya La Liga itashuhudia Getafe ikishuka uwanjani kukipiga na Real Oviedo, wakati Real Madrid itakuwa ugenini kukipiga na Real Sociedad, huku Athletic Bilbao ikiwa na kazi mbele ya Alaves na Atletico Madrid itacheza na Villarreal.
Jumapili, Celta Vigo itacheza na Girona, wakati Levante itakipiga na Real Betis, Osasuna na Rayo Vallecano wakati Barcelona ya supastaa Lamine Yamal itakuwa nyumbani kukipiga na Valencia.
Ujerumani kwenye mikikimiki ya Bundesliga, kasheshe la Jumamosi litashuhudia FC Heidenheim ikiwa nyumbani kucheza na Borussia Dortmund, Freiburg itacheza na VfB Stuttgart, Mainz 05 na RB Leipzig, wakati Union Berlin itakipiga na Hoffeinheim, Wolfsburg itacheza na FC Cologne na mabingwa watetezi, Bayern Munich watakuwa nyumbani kucheza na Hamburger SV.
Jumapili kutakuwa na mechi mbili na St Pauli itakipiga na Augsburg, wakati Borussia Monchengladbach itakuwa nyumbani kucheza na Werder Bremen. Ni balaa zito huko kwenye Bundesliga.
Kwenye Ligi ya Italia, Serie A, Jumamosi kutakuwa na mechi tatu, tu na Cagliari itajitupa nyumbani kucheza na Parma, wakati shughuli pevu itakuwa baina ya Juventus na Inter Milan zitakazoonyesha kazi ya kibabe kabla ya mabingwa watetezi, Napoli kuwa ugenini kukipiga na Fiorentina.
Jumapili kutakuwa na mechi tano huko kwenye Serie A na AS Roma itacheza na Torino, Atalanta itaonyeshana kazi na Lecce, wakati Pisa na Udinese hapatoshi kabla ya Sassuolo kucheza na Lazio na AC Milan itakuwa nyumbani kumalizana na Bologna. Kazi ipo.
Huko kwenye ligi ya Ufaransa, Ligue 1, kwa Jumamosi kutakuwa na mechi mbili tu na Nice itakipiga na Nantes, wakati Auxerre itaonyesha ubabe na AS Monaco.
Jumapili kutakuwa na mechi sita na wababe Lille watakuwa nyumbani kucheza na Toulouse, wakati Brest itakipiga na Paris FC, huku Metz ikicheza na Angers na mabingwa watetezi Paris Saint-Germain itakipiga na Lens.
Strasbourg itakuwa nyumbani kucheza na Le Havre kabla ya Rennes kumalizana na Lyon katika moja ya mechi matata kabisa kwenye mchakamchaka huo wa kusaka ubingwa wa Ufaransa msimu huu.