Ukimtaka Ronaldo kila saa ni Sh696 milioni

Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40, ambaye kwa sasa anaichezea Al-Nassr baada ya kujijengea jina kwa kucheza na timu kibao ikiwemo Sporting CP, Manchester United, Juventus, Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno, pia itakuhitaji kulipa Pauni 1.6 milioni ambazo ni zaidi ya bilioni tatu za Kitanzania ili kupata nafasi ya kuchapishiwa tangazo lako katika ukurasa wake wa Instagram ambao una wafuasi wanaofikia milioni 650.
RIYADH, SAUDI ARABIA: KITABU cha Football Leaks ambacho kimekuwa kikitoa taarifa za ndani kuhusiana na masuala ya mpira wa miguu, kimefichua kuwa ili kumpata staa wa Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo kwa ajili ya mazungumzo ya kibiashara tu, kila saa moja utatakiwa kumlipa Pauni 204,000 ambazo ni zaidi ya Sh696 milioni.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 40, ambaye kwa sasa anaichezea Al-Nassr baada ya kujijengea jina kwa kucheza na timu kibao ikiwemo Sporting CP, Manchester United, Juventus, Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno, pia itakuhitaji kulipa Pauni 1.6 milioni ambazo ni zaidi ya bilioni tatu za Kitanzania ili kupata nafasi ya kuchapishiwa tangazo lako katika ukurasa wake wa Instagram ambao una wafuasi wanaofikia milioni 650.
Kitabu cha Football Leaks kilichochapishwa na waandishi wa Der Spiegel, Rafael Buschmann na Michael Wulzinger, kilifunua maelezo kuhusu ni kiasi gani kinachotakiwa kumlipa mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or ambacho kilionyesha kuwa kampuni mojawapo ya mawasiliano ya Saudi Arabia, ilifanya makubaliano na kampuni ya haki za picha ya Ronaldo ya Uiris, Multisports & Image Management juu ya kumtumia staa huyo kwa saa nne.
Saa nne hizo zilijumuisha upigaji picha, jezi tano alizosaini na matangazo mawili kwenye mitandao yake ya kijamii, ambapo inasemekana anapata takriban Pauni 1.6 milioni kwa kila chapisho.
Ronaldo na wawakilishi wake wanadaiwa kuwa walilipwa Pauni 920,000 kwa huduma hizo zilizotajwa.
Kiasi hicho kinawiana na Pauni 204,000 kwa kila saa, Pauni 3,407 kwa kila dakika na Pauni 56.78 kwa kila sekunde aliyotumia kutoa huduma hizo.