Osimhen akubali kubaki Galatasaray kwa mkopo

Muktasari:
- Hadi sasa Napoli imeeleza kuwa haijapata ofa yoyote kutoka timu za barani Ulaya zinazohusishwa na fundi huyu na kocha wao Antonio Conte ameweka wazi kwamba hana mpango wa kumtumia Mnigeria huyo.
MSHAMBULIAJi wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria, Victor Osimhen yuko tayari kusaini mkataba wa kudumu wa kuitumikia Galatasaray ambayo aliichezea kwa mkopo msimu uliopita.
Hadi sasa Napoli imeeleza kuwa haijapata ofa yoyote kutoka timu za barani Ulaya zinazohusishwa na fundi huyu na kocha wao Antonio Conte ameweka wazi kwamba hana mpango wa kumtumia Mnigeria huyo.
Hata hivyo, ili kumpata, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Uturuki watalazimika kulipa pauni 65 milioni kwa Napoli ili kuvunja mkataba wake.
Kiasi hicho cha pesa kinaonekana kuwa kikubwa kwa Galatasaray ambayo kwa sasa imetuma maofisa wake kwenda jijini Naples ili kuzungumza na viongozi wa Napoli na kuwashawishi wapunguze bei.
Mabosi wa Galatasaray wamevutiwa sana na kiwango ambacho mshambuliaji huyu alionyesha msimu uliopita ambapo alifunga mabao 37 katika mechi 41 za michuano yote.
Mkopo wa Osimhen Galatasaray umeisha rasmi, lakini bado hana timu.
Galatasaray hawana uwezo wa kumnunua moja kwa moja, na Napoli hawamtaki tena.
Mashabiki wa Napoli pia keshawatumbuka nyongo, wakimwona kama msaliti.
Anatarajiwa kurudi kwa lazima kwa ajili ya vipimo vya afya kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya – hali inayoweza kuwa ya aibu na mvutano. Napoli imepunguza bei yake asije kuondoka bure 2026.
Matt O’Riley
AS Roma inataka kumsajili kiungo wa kati wa Brighton na timu ya taifa ya Denmark, Matt O’Riley, 24, katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Benchi la ufundo la Roma limevutiwa sana na kiwango alichoonyesha staa huyu katika dirisha lililopita ambapo alicheza mechi 26 za michuano yote.
Roma inapambana kurudi katika makali yake ya kutisha Italia na katika michuano ya Ulaya.
Anton Stach
LEEDS ina nia ya kumsajili kiungo wa kati wa Hoffenheim, Anton Stach, 26, lakini inakumbana na upinzani mkali kutoka baadhi ya timu nyingine za England ambazo zinahitaji saini yake.
Anton ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 39 za michuano yote.
Jamie Vardy
MKURUGENZI wa michezo wa Genoa, Flavio Ricciardella, alikuwa amefanya mazungumzo na wakala wa straika wa zamani wa Leicester City, Jamie Vardy na alishafikia makubaliano ya kumsajili staa huyo lakini ripoti zinaeleza kocha wao Patrick Vieira alikataa uhamisho huo wa mshambuliaji huyo wa zamani wa England mwenye umri wa miaka 38, ambaye aliachwa na Leicester wiki iliyopita.
Mathias Kvistgaarden
NORWICH imefikia makubaliana ya kumsajili beki wa Brondby na tiimu ya taifa ya Denmark mwenye umri wa miaka 23, Mathias Kvistgaarden katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Mkatana wa sasa wa Mathias unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 38 za michuano yote na kufunga mabao 23.
Malik Tillman
BAYER Leverkusen ipo katika hatua nzuri ya kumsajili kiungo wa PSV Eindhoven na timu ya taifa ya Marekani, Malik Tillman, 23, katika dirisha hili kwa ada ya uhamisho ya Euro 35 milioni.
Inaelezwa mabosi wa Leverkusen wanamwangalia fundi huyu kama mbadala wa Florian Wirtz ambaye imemuuza kwenda Liverpool katika dirisha hili.
Neil El Aynaoui
ASTON Villa inakabiliana na ushindani kutoka kwa timu mbili za Italia ambazo ni Juventus na Lazio juu ya mpango wao wa kutaka kumsajili kiungo wa Lens, Neil El Aynaoui, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Morocco chini ya miaka 23. Villa imeshatuma wawakilishi wake kwenda Ufaransa tangu mwanzoni mwa wiki hii kwa ajili ya mazungumzo.
Dusan Vlahovic
JUVENTUS bado imewaweka sokoni mshambuliaji wa kimataifa wa Serbia, Dusan Vlahovic, mwenye umri wa miaka 25, pamoja na kiungo wa kimataifa wa Brazil, Douglas Luiz, mwenye umri wa miaka 27, ili katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Awali, ilielezwa walikuwa wakifikiria kufanya mabadilishano na Man United kwa ajili ya kumsaini winga wa timu hiyo, Jadon Sancho.