Prime
Kufuru, huu hapa mshahara wa Ibenge Azam

MAMBO ni bambam kwa Wanalambalamba Azam FC baada ya kumalizana na aliyekuwa kocha mkuu wa Al Hilal Omdruman ya Sudan, Florent Ibenge, inayokipiga katika Ligi Kuu Mauritania kwa sasa, kwani ameshatia maguu Chamazi, Dar es Salaam.
Lakini, kama unataka kujua nini amedhamiria kukifanya kocha huyo ndani ya chama hilo, endelea kusikilizia kwa sasa, ingawa amegusia tu ishu ya nidhamu, ilhali masuala kama usajili na mengineyo yakiwa katika mipango yake.
Wakati hayo yote yakiwa ndo habari ya mjini kwa sasa, Ibenge ameanza mipango ya kuisuka timu hiyo kwa msimu ujao, huku ikifichuka, atakuwa akivuta kiasi cha Sh130 milioni kwa mwezi.
Ibenge ambaye ni mmoja wa makocha wakubwa Afrika amejiunga na Azam kwa ajili ya msimu wa 2025-2026 akipewa mkataba wa mwaka mmoja na kudhihirisha kukua kwa Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, imebainika kuna ushawishi mkubwa sana wa pesa nyuma ya ujio wa Ibenge.
Kocha huyo raia wa Ufaransa mwenye asili ya DR Congo, alihitajika na Azam kwa muda mrefu.
Harakati za Azam kupata huduma ya Ibenge zilianza mwaka 2020 baada ya kumtumia Aristica Cioaba, raia wa Romania.
Lakini wakati huo Ibenge alikuwa akiifundisha AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo.
Azam ikatuma mtu hadi Kinshasa kuongea na Ibenge, ambaye aliweka masharti mawili.
Kwanza masilahi yake. Alisema AS Vita ilikuwa ikimlipa Dola 15,000 (zaidi ya Sh39 milioni) na timu ya taifa ilimlipa pia kiasi kama hicho, yaani Dola 15,000.
Kwa hiyo ili aache kazi zote mbili anatakiwa apewe mshahara zaidi ya Dola 30,000 (zaidi ya Sh79 milioni) na iwapo kama atalipwa kiasi hicho cha Dola 30,000 bora akabaki hapo hapo.
Pili akasema kama Azam iko tayari kwa sharti la kwanza, basi itabidi wamsubiri hadi mwisho wa msimu kwa sababu timu yake ya Vita ilifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wakati huo na asingeweza kuiacha njiani.
Hiyo ilikuwa Desemba 2020 na Azam ilihitaji kocha muda huo, isingeweza kusubiri hadi Mei msimu utakapoisha...ndipo ikamchukua George Lwandamina kutoka Zambia.
Mawasiliano ya Ibenge na Azam yaliendelea na hata alipokuwa akija hapa nchini na Al Hilal ya Sudan aliyojiunga nayo akitokea RS Berkane mwaka 2022, alikaribishwa Chamazi kufanya mazoezi.
Upendo huo ndio uliomfanya atamani kufanya kazi na klabu hii, lakini suala la masilahi lilikuwa muhimu zaidi.
RS Berkane ilimtoa Ibenge kutoka AS Vita kwa mshahara wa Dola 40,000 (zaidi ya 105 milioni) kwa mwezi, ikiwa imeuzidi ule wa Dola 30,000 alioupata kutoka AS Vita na timu ya taifa ya DR Congo.
Kisha Al Hilal ikampata kwa dau kubwa zaidi, Dola 50,000 ( zaidi ya Sh130 milioni) kwa mwezi, yaani uliuzidi hata ule aliokuwa akilipwa ya Berkane.
Lakini Ibenge hakuwahi kufurahia maisha na Al Hilal kwa sababu ya machafuko ya Sudan.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vikasababisha timu hiyo kuishi uhamishoni kwa muda mrefu. Msimu uliomalizika hivi karibuni ilikuwa Mauritania na kucheza ligi ya nchi hiyo ikibeba taji.
Tangu ajiunge nayo, familia yake aliiacha Morocco huku akiishi kwa kuhama hama.
Zaidi ilikuwa maisha ya hotelini kila siku ilhali yeye alitaka kuishi nyumbani na familia.
Kwa hiyo alihitaji sana kuondoka Al Hilal, lakini sio kwa kuacha mshahara wake mnono, ndipo Azam wakafika kukumbushia nia yao ya mwaka 2020.
Ibenge akasema yuko tayari kufanya kazi Tanzania na mkataba wake ungeisha Juni 30, 2025, lakini anatakiwa alipwe mshahara usiopungua ule anaolipwa na Al Hilal, yaani Dola 50,000.
Wakati Azam inamfuata, Al Hilal ilishamwekea ofa ya mkataba mpya mezani, akawaonyesha Azam.
Kwa kuwa iliihitaji huduma yake, ikakubali kutoboka mfuko, hivyo Ibenge atalipwa mshahara wa Dola 50 000 kwa mwezi na Azam (zaidi ya Sh130 milioni) na kumfanya awe mmoja ya makocha wanaolipwa mshahara mnono kwa klabu za Tanzania na Afrika.