Ujerumani yatoa onyo Euro 2024

Muktasari:

  • Kikosi hicho cha Kocha Julian Nagelsmann kilianza kwa kasi kubwa na hadi mapumziko tayari kilikuwa kimeshafunga mara tatu, shukrani kwa mabao ya Florian Wirtz, Jamal Musiala na Kai Havertz, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.

MUNICH, UJERUMANI: WENYEJI wa fainali za Euro 2024, Ujerumani imetoa onyo kali kwenye mikikimikiki hiyo baada ya kuangusha kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Scotland katika mchezo wa kwanza wa fainali hizo uliofanyika Ijumaa.

Kikosi hicho cha Kocha Julian Nagelsmann kilianza kwa kasi kubwa na hadi mapumziko tayari kilikuwa kimeshafunga mara tatu, shukrani kwa mabao ya Florian Wirtz, Jamal Musiala na Kai Havertz, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.

Staa huyo wa Arsenal alifunga penalti hiyo baada ya Ryan Porteous kumchezea rafu mbaya Ilkay Gundogan na kuonyeshwa kadi nyekundu, huku Scotland iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani, kushindwa kuhimili kabisa vishindo vya wenyeji hao, wakiruhusu nyavu zao kuguswa mara mbili tena kwenye kipindi cha pili kupitia kwa Niclas Fullkrug na Emre Can, huku Antonio Rudiger akijifunga na kuwapa Scotland bao la kujifariji.

Kipute hicho kilifanyika kwenye Uwanja wa Allianz Arena na Die Mannschaft walionyesha kwamba hawataki mchezo na kutuma meseji kwamba wanachotaka ni kulibakiza kombe hilo kwenye ardhi yao ya nyumbani.

Ujerumani ilikuwa na kiwango bora kabisa kwenye mchezo huo, huku viungo wao Toni Kroos, Gundogan na Joshua Kimmich wakifanya mambo makubwa ndani ya uwanja, huku Havertz akionyesha kiwango bora kabisa, akifunga na kuasisti kwenye kiwango cha mchezaji bora wa mechi.

Ujerumani imepangwa kwenye Kundi A pamoja na timu za Hungary na Uswisi, ambazo zilitarajia kumenyana Jumamosi kwenye mchezo wao wa kwanza wa mikikimikiki hiyo ya kusaka ubingwa wa Ulaya.

Katika mchezo ujao, Ujerumani itakipiga na Hungary uwanjani MHPArena, Stuttgart, Juni 19, wakati Scotland itakuwa na kibarua kizito ikijaribu kuweka mambo sawa baada ya kipigo cha kutisha kwenye mechi yao ya kwanza kwa kukabiliana na Uswisi huko Cologne.