Manchester United yataja bei ya kumuuza Sancho

Muktasari:
- Timu inayoonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuipata saini yake inadaiwa kuwa ni Juventus lakini hadi sasa haijawasilisha ofa yoyote kwa ajili yake.
MANCHESTER United inataka Pauni 25 milioni kwa ajili ya kumuuza winga wake Jadon Sancho katika dirisha hili la majira ya kiangazi ambapo timu kadhaa zinadaiwa kuhitaji huduma yake.
Timu inayoonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuipata saini yake inadaiwa kuwa ni Juventus lakini hadi sasa haijawasilisha ofa yoyote kwa ajili yake.
Awali, ilielezwa kuwa Sancho huenda angejiunga na Chelsea kwa mkataba wa kudumu baada ya kuitumikia kwa mkopo msimu uliopita lakini matajiri hao wa Jiji la London waliamua kutomsainisha mkataba wa kudumu.
Mkataba wa sasa wa Sancho unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, msimu uliopita alicheza mechi 42 za michuano yote, akafunga mabao matano na kutoa asisti 10.
Cristian Romero
ATLETICO Madrid iko tayari kufanya kila iwezalo kumsajili beki wa Tottenham na timu ya taifa Argentina, Cristian Romero, mwenye umri wa miaka 27, katika dirisha hili la uhamisho la majira ya kiangazi.
Inaelezwa vigogo hao kutoka Madrid wanataka kuwasilisha ofa ya Pauni 61 milioni kama ada ya uhamisho kwa ajili ya kupata huduma yake kiasi ambacho Spurs wapo tayari kukipokea.
Mohammed Kudus
WEST Ham imekataa ofa ya Pauni 50 milioni kutoka kwa Tottenham kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji wao wa kimataifa wa Ghana, Mohammed Kudus, mwenye umri wa miaka 24.
Ripoti zinadai West Ham haina mpango wa kumuuza staa huyo kwa sasa lakini inaweza kufanya hivyo ikiwa timu zinazomhitaji zitawasilisha ofa inayoanzia Pauni 70 milioni. Mkataba wa Kudus unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Ademola Lookman
KOCHA wa Napoli, Antonio Conte, amewasilisha jina la mshambuliaji wa Atalanta na timu ya taifa ya Nigeria, Ademola Lookman, kwa mabosi wa timu yake na kutaka staa huyo mwenye umri wa miaka 27, asajiliwe katika dirisha hili. Conte anahitaji huduma ya Lookman kwa ajili ya kuboresha zaidi eneo la ushambuliaji la timu hiyo kuelekea msimu ujao ili kuhakikisha wanatetea taji lao.
James Trafford
NEWCASTLE inatarajia kukamilisha usajili wa kipa wa Burnley, James Trafford, mwenye miaka 22, mapema wiki ijayo baada ya kufikia makubaliano na mchezaji mwenyewe pamoja na timu yake.
Trafford ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu uliopita alicheza mechi 45 za michuano yote.
Anthony Elanga
MAZUNGUMZO baina ya wawakilishi wa Newcastle United na Nottingham Forest juu ya winga wa kimataifa wa Sweden, Anthony Elanga bado yanaendelea na ripoti zinaeleza kuna uwezekano mkubwa Elanga mwenye miaka 23, akatua Newcastle katika dirisha hili.
Mkataba wa Elanga unamalizika mwaka 2028. Mabosi wa Newcastle wamevutiwa sana na kiwango chake alichoonyesha msimu uliopita.
Ciro Immobile
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Italia anayeichezea Besiktas ya Uturuki, Ciro Immobile, mwenye miaka 35, anatarajia kuvunja mkataba wake na timu hiyo na kujiunga na Bologna bila ada ya uhamisho.
Katika msimu uliopita Ciro alicheza mechi 41 za michuano yote na kufunga mabao 19. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani.
Kaoru Mitoma
WINGA wa Brighton na timu ya taifa ya Japan, Kaoru Mitoma, 28, ameiambia timu hiyo kuwa bado anahitaji kuendelea kusalia klabuni hapo na atasaini mkataba mpya licha ya kuhusishwa na vigogo mbalimbali barani Ulaya ikiwamo Bayern Munich. Hii inakuwa ni mara nyingine kwa staa huyu kukataa ofa ya kuondoka. Alifanya hivyo pia Januari mwaka huu.