Trent kuruhusiwa fasta Madrid

Muktasari:
- Tangu Desemba mwaka jana, Real Madrid ilihitaji huduma ya beki huyo akakipige kwenye kikosi chao wakati wa fainali hizo za Fifa zitakazoanza mwezi ujao.
LIVERPOOL, ENGLAND: BEKI wa kulia, Trent Alexander-Arnold anajiandaa kwenda kujiunga na Real Madrid akitokea Liverpool kwa ada isiyozidi Pauni 1 milioni ndani ya muda ili akakipige kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu.
Tangu Desemba mwaka jana, Real Madrid ilihitaji huduma ya beki huyo akakipige kwenye kikosi chao wakati wa fainali hizo za Fifa zitakazoanza mwezi ujao.
Na ripoti kutoka Hispania zinafichua kwamba mabosi wa Liverpool wanajiandaa kumruhusu mchezaji huyo kuondoka kwa maana ya kukubali ada hiyo ya uhamisho, huku wao wakiwa na faida ya kuokoa mshahara wa mwezi mmoja wa Mwingereza huyo.
Licha ya kuwapo na maelezo kwamba Alexander-Arnold anaweza kuungana na Mohamed Salah na Virgil van Dijk kusaini dili jipya, lakini Liverpool imeonekana kutokuwa na mpango wa kubaki na mchezaji huyo, hivyo itamruhusu kwenda Bernabeu.
Mkataba wake utafika tamati Juni 30, lakini Real Madrid inataka kumpata mchezaji huyo kabla ya muda huo. Mwaka huu, dirisha la usajili la majira ya kiangazi litafanyika mara mbili — kutoka Juni 1 hadi Juni 10 na kisha Juni 27 hadi Julai 3 ili kuziruhusu klabu zitakazoshiriki kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu kuboresha vikosi vyao.
Real Madrid ipo tayari kulipa Pauni 850,000 kumsajili Trent kabla ya mkataba wake kufika ukomo ili awahi kuitumikia timu hiyo kwenye mechi yao ya kwanza dhidi ya Al-Hilal ya Saudi Arabia, Juni 18.
Wakati huo huo, Liverpool iko tayari kumpa mkataba mpya mshambuliaji Luis Diaz ili aendelee kubaki Anfield kwa muda mrefu. Staa huyo wa Colombia amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa na amekuwa akihusishwa na klabu za Barcelona na za Saudi Arabia. Diaz, 28, amekuwa na msimu bora kabisa kwenye kikosi cha Liverpool kilichonyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.