MAGUIRE: Kumbe jamaa ana mkwanja wa maana

Muktasari:
- Jina lake halisi ni Jacob Harry Maguire, alizaliwa Machi 5, 1993. Ni mwanasoka wa kulipwa, anayecheza nafasi ya beki wa kati kwenye klabu ya Manchester United inayocheza Ligi Kuu England na timu ya taifa ya England, Three Lions.
MANCHESTER, ENGLAND: HARRY Maguire. Jina maarufu sana kwa mashabiki wa soka, hasa kwa wale wafuatiliaji wa Ligi Kuu England. Anafahamika vyema. Ni beki wa boli.
Jina lake halisi ni Jacob Harry Maguire, alizaliwa Machi 5, 1993. Ni mwanasoka wa kulipwa, anayecheza nafasi ya beki wa kati kwenye klabu ya Manchester United inayocheza Ligi Kuu England na timu ya taifa ya England, Three Lions.
Maguire alikuwa gumzo kubwa baada ya kiwango chake kushuka na kuonekana kufanya makosa mengi kwenye mechi za Man United, lakini kwa sasa amekuwa gumzo tena, akibadilika na kucheza soka la kibabe kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.
Maguire alipambana kuokoa ajira yake kwenye kikosi cha Man United, ambayo inamwingizia mkwanja mrefu sana.
Kwa mkwanja ambao anavuna Old Trafford, Maguire anabaki kuwa mmoja wa wachezaji wa Ligi Kuu England wenye kipato kikubwa, akiwa na pato linalokadiliwa kuwa Pauni 24 milioni.

Uhamisho wake wa kutua Man United akitokea Leicester City mwaka 2019 ulikuwa wa pesa nyingi, Pauni 80 milioni, ambayo iliweka rekodi ya dunia kwa upande wa mabeki. Mwaka 2014, alihamia Hull City kwa ada ya Pauni 2.5 milioni, kabla ya kutolewa kwa mkopo Wigan Athletic 2015.
Alijiunga na Leicester City 2017 kwa ada ya Pauni 12 milioni na msimu wa 2017–18 alicheza kila dakika katika ligi na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu.
Man United ilivutiwa na kumnasa Maguire kwa Pauni 2019 kwa Pauni 80 milioni na ndani ya miezi sita, alichaguliwa kuwa nahodha wa kikosi hicho hadi 2023 alipovuliwa.
Maguire ana pesa, Pauni 24 milioni si ndogo.

Anapigaje pesa?
Maguire anaripotiwa kulipwa mshahara wa Pauni 190,000 kwa wiki. Kwa mujibu wa mtandao wa Spotrac, mshahara wa Maguire ni Pauni 189,904 kwa wiki na sawa na Pauni 9,875,000 kwa mwaka.
Maguire alikusanya pesa za kutosha pia alipokuwa King Power kwenye kikosi cha Leicester City, huku kipato chake kiliongezeka kila mwaka. Man United ndiyo mahali ambako amepiga pesa nyingi, aliposaini dili la miaka sita lenye mkwanja mrefu, akivuna Pauni 26,867 kwa siku.
Kwa kiwango anacholipwa Maguire kinamfanya kuwa ndani ya 10 bora ya wanasoka wanaolipwa kibosi Man United.

Mke na familia
Maguire ameoa mke mrembo, anayeitwa Fern Hawkins. Wanandoa hao wamefanikiwa kupata watoto wawili pamoja.
Lillie Saint Maguire alizaliwa Aprili 2019 na binti yao wa pili, Piper Rose, alizaliwa Mei 2020.
Mwaka 2021, walisherehekea miaka 10 ya uhusiano wao. Wawili hao walianza wakati Maguire akiwa na umri wa miaka 18 na mrembo Fern akiwa na miaka 16, walichumbiana kwenye mtoko wao huko Paris, Ufaransa mwaka 2018.
Na walifunga ndoa Ufaransa, 2022. Wawili hao walikulia Sheffield. Mwaka 2017, mrembo Fern, alihitimu shahada yake ya kwanza ya sayansi na fiziotherapia.
Maguire pia ana ndugu zake watatu. Wakiume wawili, Joe na Laurence, nao ni wanasoka. Joe anachezea Tranmere Rovers, wakati Laurence anachezea Chesterfield. Maguire ana dada pia, mrembo Daisy.
Daisy naye ni mwanasoka ana anchezea timu ya wanawake Handsworth Parramore Ladies na Sheffield United.

Makazi na usafiri
Ukicheza kwenye moja ya klabu tajiri duniani hiyo ina maana hata makazi yako yatakuwa na ubora mkubwa.
Maguire ni miongoni mwa wachezaji wenye makazi bora na anatumia usafiri mzuri pia, ndinga za maana. Maguire anaishi kwenye jumba lenye thamani ya Pauni 4 milioni.
Kuhusu usafiri, Maguire amekuwa akionekana akiendeesha magari ya kifahari kama Range Rover Sport, Audi A5 na BMW 8 Series.