Trent aambiwa aondoke Real Madrid kwa raha zake
Muktasari:
- Beki huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akisumbuliwa na majeraha tangu alipojiunga na klabu hiyo ya Bernabéu mwaka uliopita.
MADRID, HISPANIA: BEKI wa kulia, Trent Alexander-Arnold amefanya mazungumzo na kocha wa Real Madrid, Alvaro Arbeloa na kuambiwa kwa usalama wake tu, anapaswa kuondoka kwenye kikosi hicho kwa raha zake mwishoni mwa msimu.
Beki huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akisumbuliwa na majeraha tangu alipojiunga na klabu hiyo ya Bernabéu mwaka uliopita.
Na kwa mujibu wa El Nacional, Alexander-Arnold ameambiwa aondoke Real Madrid kwa faida yake mwenyewe.
Inadaiwa alionyeshwa wazi hayupo kwenye mipango ya baadaye ya vigogo hao wa LaLiga katika mazungumzo yaliyoelezwa kuwa ya kushangaza na Arbeloa. Bosi huyo wa Real Madrid pia aliweka wazi Alexander-Arnold hatapewa nafasi ya kucheza mara kwa mara atakaporejea baada ya jeraha la mguu alilopata mwezi uliopita.
Benchi la ufundi linaamini mchezaji huyo wa England hajawahi kuzoea kikamilifu maisha ya Hispania. Pia wamekuwa na wasiwasi kutokana na kiasi cha nyakati alivyokuwa akiachwa wazi kiulinzi, pamoja na kushindwa kwake kuleta mchango mkubwa wa kushambulia.
Alexander-Arnold amecheza mechi 16 pekee Real Madrid tangu aingie, akianza safari yake katika Kombe la Dunia la Klabu na ameweza kutoa asisti tatu tu.
Los Blancos ilikuwa ikitarajia mchango mkubwa zaidi, hasa kutokana na historia yake ya kuwa tishio kubwa kupitia mipira yake hatari alipokuwa Liverpool.
Hali ya Alexander-Arnold sasa imefikia kilele cha mgogoro, baada ya watu wenye ushawishi nyuma ya pazia kuamua kuwa ni bora kumuuza mwishoni mwa msimu. Hata hivyo, kiwango cha ada ambacho Real Madrid itataka bado hakijulikani, hasa baada ya kuweka kifungu cha ajabu cha kuvunja mkataba cha Pauni 840 milioni. Wawakilishi wa Alexander-Arnold tayari wameanza kutafuta klabu mbadala, wakijaribu kwa haraka kufufua upya taaluma yake.
Mshahara wake, unaodhaniwa kuwa karibu Pauni 280,000 kwa wiki, unaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa timu zinazomvizia.
Kabla ya kuondoka Anfield, Alexander-Arnold aliichezea Liverpool mara 354, akifunga mabao 23 na kutoa asisti 92.