Trent ni majanga baada majanga
Muktasari:
- Staa huyo wa zamani wa Liverpool amekuwa na wakati mgumu kwenye maisha yake ya mwanzo huko Bernabeu ambapo Septemba alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya misuli ya paja.
MADRID, HISPANIA: BEKI wa kulia, Trent Alexander-Arnold atakuwa nje ya uwanja kwa muda usiopungua miezi miwili baada ya kuumia mguu wakati wa mchezo wa Real Madrid ilipoichapa Athletic Bilbao mabao 3-0.
Staa huyo wa zamani wa Liverpool amekuwa na wakati mgumu kwenye maisha yake ya mwanzo huko Bernabeu ambapo Septemba alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya misuli ya paja.
Majeraha hayo yalimweka nje ya uwanja kwa mwezi mmoja na hivyo kumfanya akose utimamu wa mechi na hivyo kuishia kucheza mechi tano tu alizoanzishwa kwenye LaLiga msimu huu.
Na Trent sasa atakuwa kwenye huzuni kubwa baada ya kupata tatizo jingine hasa katika kipindi hiki akianza kujitafuta na kupata nafasi chini ya kocha Xabi Alonso.
Alirejea uwanjani mwanzoni mwa mwezi uliopita na alianzishwa kwenye kikosi cha Los Blancos katika mechi nne zilizopita. Alionyesha kiwango bora dhidi ya Bilbao, ambapo aliasisti bao la kwanza lililofungwa na Kylian Mbappe.
Lakini, alilazimika kutoka uwanjani baada ya kupata maumivu ya paja katika dk10 baada ya kuanza kipindi cha pili na nafasi yake kuingizwa Raul Asencio. Majeraha hayo ni habari mbaya kwa kocha Alonso, ambaye pia anakosa huduma ya beki wa kulia, veterani Dani Carvajal hadi mapema mwakani.
Federico Valverde anatarajia kutumika kama kiraka.