Trent anataka kuondoka Madrid
Muktasari:
- Trent alijiunga na Real Madrid dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kwa ada ya uhamisho ya Pauni 10 milioni ambayo mabingwa hao wa Hispania waliilipa ma kumsajli kabla ya mkataba wake kumalizika ili awatumikie katika michuano ya Kombe la Dunia la klabu.
MADRID, HISPANIA: BEKI wa kulia wa Real Madrid, Trent Alexander-Arnold yupo katika rada za timu kadhaa Ulaya zinazohitaji kumsajili baada ya kuona hapati nafasi ya kutosha katika viunga vya Santiago Bernabeu.
Trent alijiunga na Real Madrid dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kwa ada ya uhamisho ya Pauni 10 milioni ambayo mabingwa hao wa Hispania waliilipa ma kumsajli kabla ya mkataba wake kumalizika ili awatumikie katika michuano ya Kombe la Dunia la klabu.
Katika michuano hiyo, Trent alicheza mechi tano na tangu kuanza kwa ligi hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa na alikuwa akisugua benchi chini ya Kocha Xabi Alonso.
Inaelezwa, Trent ambaye msimu huu amecheza mechi nane tu za La Liga, yupo katika orodha ya mastaa ambao Madrid inafikiria kuwauza ikiwa ofa nzuri itawasilishwa katika dirisha hili au lijalo.
Tovuti ya Fichajes inaeleza hali ya kutofikia malengo kutokana na majeraha ya mara kwa mara na kuonyesha kiwango cha chini hata pale alipokuwa anapata nafasi ya kucheza, imewafanya mabosi wa Madrid kuamini staa huyo ameshindwa.
Mbali ya Madrid, Trent mwenyewe pia anadaiwa kutofurahia maisha yake katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na anaona anahitaji kuondoka ili kurudisha kiwango chake sehemu nyingine.
Ripoti zinadai mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 yupo kwenye rada za Bayern Munich, ambayo inazungumza na wakala wake kuona namna ambavyo inaweza kumpata.
Ingawa alisaini mkataba wa miaka sita, kutokuwa na furaha kwake kumefungua fursa ambayo Bayern hawataki kuipoteza na kocha wa timu hiyo, Vincent Kompany ameeleza upande wa kulia ni eneo muhimu la kuimarisha kwenye kikosi chake na anaona Alexander-Arnold kama mtu sahihi ikiwa ataipata huduma yake.
Mbali ya Bayern, huduma ya staa huyu pia inahitajika na Newcastle United, timu ambayo imemhakikishia nafasi ya kuwa mchezaji kinara katika kikosi chao ikiwa ni pamoja na kumlipa mshahara mkubwa kuliko mchezaji yeyote katika kikosi chao.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, timu zinazomhitaji staa huyu zinatakiwa kulipa Pauni 35 milioni kama ada ya uhamisho ambayo licha ya kuonekana kuwa ndogo kwa mchezaji daraja la Trent ambaye pia ana mkataba wa miaka sita, bado itakuwa ni faida kwa Madrid ukilinganisha na bei ambayo wao walimnunulia.