Ten Hag akubali yaishe kwa Sancho

Muktasari:

  • Ten Hag amefuatilia kiwango cha mchezaji huyo anachokionyesha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Dortmund, ambapo kikosi hicho cha Bundesliga kwa sasa kipo kwenye hatua ya nusu fainali.

MANCHESTER, ENGLAND. HABARI ndo hiyo. Erik ten Hag amefungua milango kwa winga Jadon Sancho kurejea Manchester United.

Kocha huyo wa Manchester United alimwondoa Sancho kwenye kikosi cha kwanza Septemba, mwaka jana, baada ya kutuma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii akijaribu kumwita Mdachi huyo kuwa ni muongo.

Kilichotokea Ten Hag alimwondoa Sancho kwenye kikosi kilichocheza na Arsenal kwa madai kwamba hakuonyesha kiwango kizuri mazoezini, jambo ambalo winga huyo wa Kingereza alisema si kweli na anageuzwa tu kuwa mbuzi wa kafara. 

Sancho aligoma kumwomba radhi kocha wake na hapo akaambiwa afanye mazoezi kivyake kabla ya kuhamishiwa kwenye mazoezi ya timu ya watoto na baadaye akatolewa kwa mkopo kwenda Borussia Dortmund kwenye dirisha la Januari.

Lakini, Ten Hag amefuatilia kiwango cha mchezaji huyo anachokionyesha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Dortmund, ambapo kikosi hicho cha Bundesliga kwa sasa kipo kwenye hatua ya nusu fainali.

Ten Hag alisema: “Ndio, nafuatilia michuano ya kimataifa kwa sababu kuna wachezaji wetu wapo kwa mkopo kwenye klabu nyingine. Sancho alikuwa na kiwango kizuri kwenye mechi ya Dortmund dhidi ya Atletico Madrid.

“Kilikuwa kiwango kizuri kutoka kwa Dortmund na alichofanya Jadon ni habari njema. Amechangia matokeo ya Dortmund.”

Kitendo cha Ten Hag kumzungumzia Sancho kimedaiwa kwamba ni dalili nzuri ya wawili hao kwamba wanaweza kumaliza tofauti zao na kufanya kazi pamoja mkali huyo atakaporejea Old Trafford.

Ten Hag alisema: “Tunafahamu Jadon Sancho ni mchezaji mahiri, hivyo hilo halitushangazi, si kitu kipya.”

Man United itakipiga na Coventry City kwenye nusu fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley, kesho Jumapili.

...