Tajiri Man United amtega Amorim

Muktasari:
- Tajiri huyo wa Man United anataka kumpa sapoti Amorim kwenye dirisha la usajili lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kunasa huduma za wachezaji watakaokuja kubadili hali ya mambo Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: MMILIKI mwenza wa Manchester United, bilionea Sir Jim Ratcliffe yupo tayari kumpatia kila kitu kocha Ruben Amorim ili kuibadili timu hiyo lakini anachotaka ni uhakika kwamba Mreno huyo anabaki.
Tajiri huyo wa Man United anataka kumpa sapoti Amorim kwenye dirisha la usajili lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kunasa huduma za wachezaji watakaokuja kubadili hali ya mambo Old Trafford.
Lakini, kauli ya hivi karibuni ya kocha Amorim imemwacha Ratcliffe kwenye wasiwasi mkubwa kwamba Mreno huyo ameshaanza kuona jukumu la kuijenga upya Man United ni ngumu sana kwake.
Amorim alisema wiki iliyopita kwamba atalazimika kung'atuka kama itahitajika kufanya hivyo baada ya karibu miezi saba ya kuinoa timu hiyo tangu aliporithi mikoba ya Mdachi, Erik ten Hag.
Alisema: "Ni suala la kufanya uamuzi kwenye historia ya klabu. Tunahitaji kuwa na nguvu kubwa katika dirisha lijalo la uhamisho wa wachezaji ili msimu ujao tusiwe kama hivi. Kama tutaanza msimu mpya tukiwa kwenye hali hii, na kama mambo yatabaki kuwa hivyo, itatupasa kutoa nafasi kwa ajili ya wengine waje."
Lakini, kabla ya kukipiga na Chelsea, Ijumaa iliyopita katika mchezo wa Ligi Kuu England, ambapo Man United ilichapwa 1-0, kocha Amorim alisema tena kwa msisitizo kwamba hawezi kung'atuka.
Kinachoelezwa ni kwamba tajiri Ratcliffe ana wasiwasi kwamba kocha huyo wa zamani wa Sporting Lisbon, Amorim anaweza kuamua inatosha na kujiweka pembeni baada ya timu hiyo kushindwa kubadilika.
Tajiri Ratcliffe anamwona Amorim kama mtu mwenye misimamo kama yake hivyo anavutiwa kufanya kazi naye. Lakini, anahitaji kuhakikishiwa kwamba atabaki kwenye kikosi cha Man United hadi mwisho wa mkataba wake ili kubadili hali ya mambo katika kikosi cha Man United.