Mastaa wa Man United washona suti za ubingwa

Muktasari:
- Kitatokea nini huko Estadio de San Mames, Bilbao, Hispania ni kitu cha kusubiri na kuona. Lakini, mastaa wa Man United wamejiandaa kwa mechi hiyo ya fainali kushona suti matata za mbunifu Paul Smith zenye thamani ya Pauni 1,000 kwa kila suti sawa na Sh3,578,290 kwa pesa ya Kitanzania.
MANCHESTER, ENGLAND: WEITA ongeza glasi. Ndivyo shangwe litakavyokuwa kwa mashabiki wa timu ambayo itakuwa imeshinda kati ya Manchester United na Tottenham Hotspur zitakazokutana kwenye fainali ya Europa League usiku wa Jumatano.
Kitatokea nini huko Estadio de San Mames, Bilbao, Hispania ni kitu cha kusubiri na kuona. Lakini, mastaa wa Man United wamejiandaa kwa mechi hiyo ya fainali kushona suti matata za mbunifu Paul Smith zenye thamani ya Pauni 1,000 kwa kila suti sawa na Sh3,578,290 kwa pesa ya Kitanzania.

Man United inataka kwenda kuwapa raha mashabiki wao baada ya kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu England kwa kubeba taji la Ulaya katika fainali hiyo ya Bilbao, usiku wa Jumatano.
Katika kipute hicho, miamba miwili ya Ligi Kuu England itachuana yenyewe na vita haitakuwa tu kubeba taji hilo, bali pia kupambana kuwania tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Spurs na Man United zote zimekuwa na msimu mbaya kwenye Ligi Kuu England, hivyo mshindi kwenye fainali hiyo atafarijika kwa matokeo hayo.

Man United inaamini yenyewe ndiyo itakayokwenda kuibuka na ushindi kwenye fainali hiyo ili kumweka pazuri Kocha Ruben Amorim, ambaye ameiongoza kushinda mechi 10 na kukusanya pointi 39 kwenye Ligi Kuu England na imebakiza mechi moja tu.
Hata hivyo, katika usiku huo matata kabisa wa Europa League, mastaa wa Man United wamehakikisha wanajiweka fiti kwenye kila kitu, ikiwamo mavazi na ndiyo maana imeshona suti maalumu za kusherehekea ubingwa.

Man United imekuwa na utamaduni wa kushona suti kabla ya mechi za fainali, tangu kipindi hicho walichokuwa wakibeba mataji karibu kila msimu ilipokuwa chini ya Kocha Sir Alex Ferguson.

Mwaka jana ilishona suti kabla ya kwenda kushinda Kombe la FA kwa kuichapa Manchester City katika mchezo wa fainali uliofanyika uwanjani Wembley. Sasa miamba hiyo ya Old Trafford itashona suti mpya, ambazo zitashonwa na dizaina Paul Smith, ambaye wamekuwa washirika tangu mwaka 2008. Mastaa kama Bruno Fernandes, Mason Mount na Harry Maguire walijaribisha kuona suti hizo zinawapendeza kiasi gani kabla ya fainali yenyewe kupigwa.
Mashabiki wa Man United wamefurahi kuona wachezaji wao wameshona suti wakiamini hiyo ni dalili nzuri watakwenda kushinda fainali hiyo na hivyo kuelezea hisia zao mtandaoni.

Shabiki wa kwanza alisema: “Tafadhali, tushinde jamani.”
Mwingine alisema: “Mmependeza vijana, twende tukashinde hii.”
Huku shabiki wa tatu alisema: “Naamini kiwango cha soka uwanjani kutaendana na kupendeza kwa mshono wa suti.” Shabiki mwingine alisema: “Mmependeza.”