Slot atoa ujumbe mzito

Muktasari:
- Liverpool walikuwa wakisherehekea kutwaa ubingwa wao wa 20 wa EPL katika mitaa ya Jiji lao, anmbapo maelfu ya mashabiki walijitokeza mitaani kuwapongeza mashujaa wao.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot, amezungumza kwa mara ya kwanza kufuatia tukio la gari kuwagonga watu wakati ya maandamano ya kusherehekea ushindi wa taji lao la Ligi Kuu England, Jumatatu jioni.
Liverpool walikuwa wakisherehekea kutwaa ubingwa wao wa 20 wa EPL katika mitaa ya Jiji lao, anmbapo maelfu ya mashabiki walijitokeza mitaani kuwapongeza mashujaa wao.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya maandamano kumalizika, gari liliingia kwa kasi kwenye kundi la watu katika mtaa wa Water katikati ya jiji la Liverpool mida ya saa 12 jioni, na kusababisha majeruhi 65.
Polisi walithibitisha Jumanne jioni kwamba mashabiki 11 bado walikuwa wakipokea matibabu hospitalini, lakini walionekana kuwa katika hali nzuri.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 53, raia Uingereza, amekamatwa kwa tuhuma za jaribio la mauaji, uendeshaji hatari, na kuendesha akiwa amelewa dawa za kulevya.
Slot alitarajiwa kuhudhuria hafla ya kila mwaka ya utoaji wa tuzo ya Chama cha Mameneja wa Ligi (LMA), lakini aliamua kutoihudhuria kutokana na tukio hilo la kusikitisha.
Hata hivyo, alitoa taarifa rasmi, akishukuru jamii ya soka kwa kuungana na Liverpool wakati huu wa huzuni.
“Kama mnavyofahamu, tukio la kushtua lilitokea Liverpool jana, ambalo liliwaacha watu waliokuwa wamehudhuria maandamano yetu wakiwa wamejeruhiwa. Kwa sababu hiyo, nimeamua kujiondoa kushiriki katika hafla ya Chama cha Mameneja kama ishara ya mshikamano na wote walioathirika,”alisema Slot.
“Huu si uamuzi niliouchukua kwa urahisi, lakini naamini ni sahihi kutokana na uzito wa hali hiyo. Natumai mtaelewa. Nataka kuwapongeza watu wa huduma za Afya na mamlaka nyingine Jijini Liverpool waliochukua hatua mara moja baada ya tukio hilo kutokea.”
Licha ya kutohudhuria sherehe, Slot alitangazwa kushinda tuzo mbili kubwa,yakwanza kuwa kocha bora wa Ligi Kuu England na Kocha Bora wa LMA wa Mwaka, baada ya kuiongoza Liverpool kutwaa ubingwa katika msimu wake wa kwanza akiwa Anfield.