Mabomu, vurugu vyatawala Chelsea ikitwaa ubingwa

Muktasari:
- Katika mchezo huo ambao Chelsea ilishinda kwa mabao 4-1 na kuchukua taji, kabla ya kuanza mashabiki waliokuwa karibu na mitaa ya Uwanja wa Miejski ilipofanyika walianzisha vurugu kwa kupigana hali iliyosababisha polisi kurusha mabomu ya moshi na maji ya kuwasha ili kutuliza ghasia hizo.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa soka kutoka Uingereza na Hispania walihusika katika mapigano ya mtaani, wakirusha chupa na kupigana ngumi saa kadhaa kabla ya mechi ya fainali ya Uefa Conference League kati ya Chelsea na Real Betis kuanza.
Katika mchezo huo ambao Chelsea ilishinda kwa mabao 4-1 na kuchukua taji, kabla ya kuanza mashabiki waliokuwa karibu na mitaa ya Uwanja wa Miejski ilipofanyika walianzisha vurugu kwa kupigana hali iliyosababisha polisi kurusha mabomu ya moshi na maji ya kuwasha ili kutuliza ghasia hizo.
Saa chache tu kabla ya mechi kuanza, mapigano yalizidi kuenea wakati mashabiki walipoanza kurushiana fataki na kuingia kwenye makambi ya wapinzani wao kwa miguu na mateke.
Mashabiki walionekana wakirushiana viti na mafataki, wakati wengine wakizichapa kavu kavu, kabla ya polisi waliokuwa na bunduki kufika na kuwatuliza.
Kwa mujibu wa video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, polisi walilazimika kutumia maji ya kuwasha ambayo yalisaidia kutuliza vurugu hizo haraka.
Chelsea walishinda fainali hiyo kwa kutokea nyuma baada ya kuongozwa kwa karibia dakika 50 kwa bao 1-0 kabla ya kuanza kusawazisha kupitia kwa nyota Cole Palmer.
Taarifa nyingine zinaeleza kwamba, mashabiki walikuwa wakipigana mitaani kwa takribani saa 24 kabla ya mechi kuanza.
Inakadiriwa kuwa mashabiki wapatao 70,000 waliwasili jijini humo mapema wiki hii, wengi wao wakinywa na kula karibu na mashabiki wa timu pinzani.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi la Mkoa wa Lower Silesia huko Wrocław ilisema kuwa watu 28 walikamatwa Jumatano kufuatia vurugu hizo.
“Kwa sasa, tunaweza kuthibitisha kuwa watu 28 wamekamatwa. Hakuna atakayepona mbele ya mkono wa sheria na polisi wataendelea kuchukua hatua madhubuti na sahihi.” ilisema taarifa ya polisi.
Video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mapigano makali mitaani katika baadhi ya baa na migahawa ya jiji hilo.
Katika kipande kimoja cha video, kundi la vijana watano lilionekana likivunja viti na kurusha glasi kwa kundi jingine lililojificha chini ya paa la jengo. Dirishani, kulikuwa na bendera kubwa ya bluu iliyoandikwa “London only”, ikionyesha huenda lilikuwa eneo la mashabiki wa Chelsea.
Kipande kingine kilionyesha makundi mawili yakirusha vitu kwa kila mmoja kutoka baa tofauti.
Vurugu kama hizo ziliripotiwa pia siku mbili kabla ya mechi ambapo gesi ya kutoa machozi ilihitajika kuwatenganisha mashabiki waliokuwa wakikabiliana katika vurugu hizo.