Slot apindua meza liverpool
Muktasari:
- Real Madrid ilikuwa mwiba wa mtangulizi wake Jurgen Klopp, licha ya mafanikio yake makubwa. Klopp alikumbana na machungu ya kupoteza fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya vigogo hao wa Hispania 2018 na 2022, pamoja na kushindwa mara mbili zaidi katika kipindi cha misimu saba iliyopita.
LIVERPOOL, ENGLAND : ARNE Slot sasa anaweza kuandikisha historia mpya kwa kufuta kumbukumbu mbaya zilizowahi kuikumba Liverpool katika miaka ya hivi karibuni, akijipatia sifa zaidi kutokana na mwanzo wake wa kuvutia kama kocha wa timu hiyo baada ya juzi kuichapa Real Madrid mabao 2-0.
Real Madrid ilikuwa mwiba wa mtangulizi wake Jurgen Klopp, licha ya mafanikio yake makubwa. Klopp alikumbana na machungu ya kupoteza fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya vigogo hao wa Hispania 2018 na 2022, pamoja na kushindwa mara mbili zaidi katika kipindi cha misimu saba iliyopita.
Hata hivyo, Slot ameibadilisha historia hiyo kwa kishindo kikubwa, akiweka kikomo kwa mfululizo wa mechi sita za kushindwa na sare mbili dhidi ya mabingwa mara 15 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ushindi huu umeonyesha nia thabiti ya Slot tangu achukue mikoba ya Klopp, jambo linalothibitisha kuwa kocha huyu wa Uholanzi, mwenye utulivu, anaweza kupenya mahali palipoonekana kuwa pagumu kupita maelezo.
Klopp alimuachia Slot kikosi bora, lakini Slot amekisuka kwa mtindo wake, wenye nidhamu lakini pia mvuto. Rekodi ya kushinda mechi 17, kupoteza moja tu na kutoka sare moja inaonyesha wazi namna kocha huyu alivyoweka alama yake Anfield.