Siyo poa! Mastaa Man United hawajafurahishwa
Muktasari:
- Wachezaji wa Man United walipewa taarifa ya kutimuliwa Amorim mapema Jumatatu asubuhi, lakini chanzo cha karibuni kinadai kwamba huko kwenye vyumba vya kubadilishia taarifa zilizopo ni kwamba wanadhani kocha alifukuzwa kazini mapema sana.
MANCHESTER, ENGLAND: NDO hivyo. Lisemwalo ni kwamba kuna kundi kubwa la mastaa wa Manchester United hawajafurahishwa na namna klabu hiyo ilivyomfuta kazi kocha Ruben Amorim.
Taarifa za kutoka ndani zinadai kwamba Amorim alikuwa maarufu kwa baadhi ya wachezaji mastaa kwenye kikosi hicho na kwamba alikuwa akipata sapoti kubwa kutoka kwao.
Wachezaji wa Man United walipewa taarifa ya kutimuliwa Amorim mapema Jumatatu asubuhi, lakini chanzo cha karibuni kinadai kwamba huko kwenye vyumba vya kubadilishia taarifa zilizopo ni kwamba wanadhani kocha alifukuzwa kazini mapema sana.
Licha ya chanzo hicho kudai kwamba Man United hakukuwa na tatizo la kocha kupoteza hadhi yake kwa wachezaji na kutoonekana na mabadiliko ya kimaendelea ndani ya uwanja, lakini kinachoelezwa panga limetua kwenye shingo ya Amorim ni kutokana na uamuzi wake wa kuwashambulia hadharani mabosi wake kwenye mkutano wa waandishi wa habari baada ya mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Leeds United, Jumapili iliyopita.
Mastaa kadhaa wa Man United wameonyesha heshima kwa Amorim kwenye mitandao ya kijamii na kusema walichokisema baada ya taarifa hiyo ya Jumatatu.
Patrick Dorgu na Benjamin Sesko walikuwa miongoni mwa wachezaji waliomtakia heri kocha huyo, licha ya chanzo kimoja ndani ya Man United kudai kwamba kuna baadhi ya mastaa walimkosoa Amorim kimyakimya kabla ya kuonyeshwa mlango wa kutokea.
Dorgu na Sesko ni miongoni ni mastaa waliosajiliwa na mabosi wa Man United, akiwamo mkurugenzi wa soka, Jason Wilcox na hawakuwa na tatizo lolote na Amorim.
Tofauti na makocha waliopita ambao walifutwa kazi Manchester United, safari hii wachezaji hawajaombwa maoni yoyote juu ya Amorim kabla ya uamuzi wa kumfukuza haujachukuliwa.
Dorgu, Sesko, Diogo Dalot, Harry Maguire, Matthijs de Ligt, Amad, Bryan Mbeumo, Mason Mount, Bruno Fernandes na Joshua Zirkzee wote walimshukuru Amorim kwenye kurasa zao za mtandao wa Instagram baada ya taarifa ya kocha huyo kufukuzwa kuandikwa.
Kulikuwa na wachezaji wanne tu wa Man United ndiyo waliomshukuru Jose Mourinho wakati alipofutwa kazi Desemba 2018. Na sasa Darren Fletcher ameteuliwa kuwa kocha wa muda.
Man United itarejea uwanjani Jumatano kukipiga na Burnley kwenye mchakamchaka wa Ligi Kuu England ugenini. Baada ya hapo itakipiga na Brighton kwenye Kombe la FA kabla ya kurudi tena kwenye ligi, ambapo itakipiga na Man City, Arsenal, Fulham na Tottenham Hotspur.
Baada ya kufutwa kazi, Amorim alionekana akiwa mtaani na mkewe wakitembelea wakiwa na uso wa bashasha baada ya kuelezwa kocha huyo Mreno ameigharimu Man United, Pauni 30 milioni. Kwa sasa Man United iko sokoni kusaka kocha.