Arsenal mpo? Sikieni hii ishu ya Arteta
Muktasari:
- Mabosi wa Old Trafford wanajikuta wakitafuta kocha mpya kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha chini ya miezi 18 baada ya kumfuta kazi Ruben Amorim siku ya Jumatatu.
LONDON, ENGLAND: RIO Ferdinand ametoa kauli ya kushangaza akidai Mikel Arteta angefikiria kuchukua kazi ya Manchester United endapo angepigiwa simu, licha ya kuwa na malengo ya muda mrefu akiwa na kikosi kinachofanya vizuri cha Arsenal.
Mabosi wa Old Trafford wanajikuta wakitafuta kocha mpya kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha chini ya miezi 18 baada ya kumfuta kazi Ruben Amorim siku ya Jumatatu.
Kocha huyo raia wa Ureno alifukuzwa kazi katikati ya mvutano baada ya kulipuka mbele ya waandishi wa habari akiwashambulia mabosi wake baada ya mechi huko Leeds United.
Darren Fletcher ataiongoza timu katikati ya wiki dhidi ya Burnley, huku mpango ukiwa ni kumteua kocha wa mpito hadi mwisho wa msimu kabla ya kumtafuta wa kudumu msimu wa kiangazi.
Majina kama Oliver Glasner na Xavi tayari yametajwa wagombea, huku tetesi kuhusu meneja ajaye wa Man United zikiongezeka. Ingawa Arteta, ambaye kwa sasa anafurahia maisha katika klabu ya zamani Arsenal, hayumo kwenye mazungumzo rasmi, swali liliulizwa kwa Ferdinand iwapo Arteta angeikataa ofa ya Man United, lakini beki huyo wa zamani wa Man United hakukubaliana na hilo.
“Hapana, sikubaliani na hilo kabisa,” amesema kwenye toleo jipya la Rio Ferdinand Presents.
“Hawezi kusema hadharani, hatawahi kusema wazi. Lakini, ninakwambia, Mikel Arteta angekaa chini na kulifikiria.” Arteta amesimamia mabadiliko makubwa Emirates tangu achukue mikoba zaidi ya miaka sita iliyopita. Hajashinda taji tangu 2020, lakini amesaidia Arsenal kurejea kwenye nguvu ndani ya uwanja Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kikosi chake kina baadhi ya wachezaji bora duniani, akiwemo Declan Rice na William Saliba.
Hajaonyesha dalili zozote za kutaka kuondoka kaskazini mwa London, na yuko katika nafasi nzuri ya hatimaye kuvunja mwiko huo huku Arsenal wakiwa mbele kwa pointi sita kileleni mwa ligi. Kombe linaonekana kuwa karibu, huku United wakihitaji kuanza upya tena kwa sababu kikosi chao kiko mbali sana na ushindani wa ubingwa.