Siri imefichuka! Matajiri Saudia wamshawishi Beckham dili la kuinunua Man United
Muktasari:
- Kundi hilo la wawekezaji ambalo bado halijatajwa jina, linadaiwa kupanga kununua hisa zinazomilikiwa na familia ya Glazer, ambao ni wamiliki wakuu wa klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 20.
Gwiji wa Manchester United, David Beckham amependekezwa kushirikiana na kundi la mabilionea kutoka UAE (Falme za Kiarabu) ambao wanapanga kuwasilisha ofa ya kuinunua klabu ya klabu hiyo, kwa mujibu wa taarifa zilizovuja.
Kundi hilo la wawekezaji ambalo bado halijatajwa jina, linadaiwa kupanga kununua hisa zinazomilikiwa na familia ya Glazer, ambao ni wamiliki wakuu wa klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 20.
Kama sehemu ya mpango huo, mabilionea hao wamemfuata Beckham ambaye aliitumikia Man United kwa mafanikio makubwa kuanzia mwaka 1992 hadi 2003, ili kumshawishi ajiunge nao kwenye mchakato wa kuwasilisha zabuni huko Old Trafford.
Kwa mujibu wa magazeti ya Star na Mirror, nyota huyo wa zamani wa United, bingwa wa Ligi Kuu mara sita na mshindi wa treble mwaka 1999, ameombwa ashikirikiane na kundi hilo, huku akishawishiwa kuwekeza endapo atapendezwa na ombi hilo.
Beckham, mwenye umri wa miaka 50 na utajiri unaokadiriwa kufikia Pauni 300 milioni, tayari anamiliki klabu ya Inter Miami na Salford City. Umaarufu wake wa kimataifa umemfanya kuwa chaguo la kwanza mbele ya vigogo wengine wa zamani wa Man United kama Eric Cantona na Wayne Rooney kwa nafasi hiyo ya uwakilishi.
Beckham amekuwa mkosoaji wa familia ya Glazer, akilalamikia uongozi wao unaodaiwa kuingiza madeni makubwa klabu hiyo, ambapo zaidi ya Pauni 1.2 bilioni zimetumika kulipa riba ya madeni, deni lenyewe, gawio, na ada mbalimbali kwa familia hiyo ya Marekani.
Ingawa thamani ya sasa ya United inakadiriwa kuwa karibu Pauni 2 bilioni, familia ya Glazer inasemekana inataka kiasi cha hadi Pauni 5 bilioni, ili kukubali kuuza sehemu hisa zao za umiliki.
Hivi sasa, Glazer bado ni wamiliki wakuu wa Man united, lakini tayari wameuza chini ya asilimia 30 ya hisa zao kwa Sir Jim Ratcliffe wa kampuni ya Ineos, aliyelipa Pauni 1.2 bilioni ambapo aliweza kuingia kwenye klabu hiyo mwaka 2023, akimshinda mpinzani wake Sheikh Jassim wa Qatar.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, vyombo vya habari vya SunSport viliripoti kuwa madai ya uwepo wa mpango mwingine wa kuinunua klabu ya Man united yamewaacha watu wa ndani wa United wakiwa na mshangao.
Afisa wa serikali ya Saudi Arabia, Turki Alalshikh, alidokeza kuwa kuna mazungumzo ya mauzo yanayoendelea kuhusu kuuzwa kwa Man United, jambo ambalo linaweza kuhusiana na bilionea Rodolphe Saadé ambaye ni mwenyekiti wa kampuni kubwa ya usafirishaji CMA CGM Group.
Kampuni hiyo imechukua umiliki wa Freightliner, ambao wanamiliki ardhi iliyo karibu na Old Trafford, eneo lililo katika mipango ya kujenga uwanja mpya wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 100,000.
Wakati hayo yote yakiendelea nje ya uwanja, kikosi cha Ruben Amorim kinasafiri kuelekea Anfield kucheza na Liverpool leo Jumapili, katika pambano kubwa la Ligi Kuu ya EPL.
United haijashinda mechi ya ugenini dhidi ya Liverpool tangu Januari 2016.