Beckham, Victoria wafichua biashara ilivyokaribia kuwafilisi
Muktasari:
- Wanandoa hao mashuhuri duniani wamefichua ukweli huo kwa mara ya kwanza, huku wakisema biashara hiyo ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Victoria Beckham iliwapotezea pesa nyingi, na walikuwa wakihangaika kuisimamia.
Gwiji wa Manchester United, David Beckham, na mkewe Victoria Beckham, wamefichua walipitia changamoto katika ndoa yao kufautia biashara ya mavazi, licha ya kuonekana ilikuwa na mafanikio makubwa, lakini haikuwa hivyo.
Wanandoa hao mashuhuri duniani wamefichua ukweli huo kwa mara ya kwanza, huku wakisema biashara hiyo ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Victoria Beckham iliwapotezea pesa nyingi, na walikuwa wakihangaika kuisimamia.
Katika makala yao ya Netflix, wanandoa hao wameeleza kwamba walikuwa na madeni ya mamilioni ya dola kutokana na biashara hiyo ya mitindo kutofanya vizuri kifedha.
Victoria alikuwa wa kwanza kufichua ukweli huo, huku akisema biashara hiyo ni kila kitu kwake, lakini haikuwa rahisi kuiendesha kwa sababu haikumpa faida yoyote kama alivyotarajia mwanzo.
"Biashara hii ni kila kitu kwangu, ni sehemu halisi ya mimi. Lakini imekuwa safari ngumu sana. Karibu nipoteze kila kitu. Ilikuwa kipindi cha giza sana. Nilikuwa nalia kila siku kabla ya kwenda kazini, kwa sababu nilihisi kama nimepoteza.
"Tulikuwa tuna deni la zaidi ya mamilioni. Nilipokuwa narudi nyumbani kwa mume wangu, lakini pia nilikuwa narudi kwa mshirika wangu wa biashara. Nililazimika kuzungumza naye kuhusu hili kwa sababu naye alikuwa amewekeza, lakini sikupendezwa sana na na hilo. Nilichukia kabisa."
Kwa upande wa David Beckham naye amekiri kuwa hali hiyo ilikuwa ngumu, na alikuwa akitafuta suluhisho la haraka kwa sababu hawakuwa na fedha za kuendeleza biashara hiyo kama ilivyokuwa.
"Tulikaa chini wote wawili, tukatazama nilichokuwa nimewekeza. Na sehemu ya mazungumzo hayo ilinivunja moyo, kwa sababu Victoria ni mwanamke mwenye kujivunia. Tulipokutana, alikuwa tajiri kuliko mimi. Yeye ndiye alinunua nyumba yetu ya kwanza kule Hertfordshire, tuliyoita Beckenham Palace."
"Kwa hiyo ilipofika hatua ya kuniambia, ‘tunahitaji pesa zaidi, biashara inahitaji pesa zaidi,’ ilikuwa ngumu kwa wote wawili. Kwa sababu mimi pia sikuwa na pesa za kuendelea kuingiza humo. Hatimaye nikasema, hatuwezi kuendelea hivi."
Biashara hiyo ya Victoria Beckham ilianza kupata nafuu baada ya kumleta David Belhassen kama mshirika. Alianzisha mpango wa kupunguza gharama na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima.
Belhassen amefichua kuwa, biashara ilikuwa katika hali tete kwa sababu Victoria na David walizungukwa na watu waliokuwa hawako tayari kuwaambia ukweli au kuwazuia kupoteza fedha.
"Nilikwenda kwa Victoria na kuamua kumwambia ukweli kama ulivyo, sikujua ataitikaje. Nikamwambia: Victoria, lazima tubadilishe kila kitu, tuimarishe upya biashara na hilo litakuwa na maumivu. Alinisikiliza tu, hakusema chochote mara moja, akanyamaza kidogo."
Mojawapo ya mambo aliyobaini ni kuwa mimea ya ofisini ilikuwa inagharimu Pauni 70,000 kwa mwaka, pamoja na Pauni 15,000 nyingine kwa mtu aliyekuwa akiziwagilia jumla ya Pauni 85,000 kwa mwaka kwa mimea pekee.
Kwa kufuata ushauri wa Belhassen na kufanya mabadiliko muhimu, David na Victoria Beckham waliweza kuiokoa biashara hiyo na kuirejesha kwenye njia ya mafanikio.