Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mitego sita inayomsubiri Manqoba Yanga

VIHUNZI Pict


WAKATI mwingine kocha mpya harithi tu mikoba ya timu, bali hurithi matarajio, presha na deni la mafanikio ndivyo ilivyo kwa Manqoba Mngqithi aliyetambulishwa kutua Jangwani siku chache zilizopita.


Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, anaingia Yanga ikiwa inashikilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini pia ikiwa kwenye kipindi kigumu cha mabadiliko ya kikosi na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki.


Kwa nje unaweza kuona amekabidhiwa timu inayotwaa mataji lakini kwa ndani anakutana na kikosi kinachoanza kujengwa upya, nyota wanaoondoka, wengine wanaumia, wapya wanaowasili na msimu unaokaribia kuanza.

Katika soka la Afrika hakuna anayepewa miezi sita ya kujifunza, matokeo yanatakiwa kuonekana kuanzia mchezo wa kwanza tu hivyo hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Manqoba atakuwa nayo kichwani wakati akiweka mipango yake sawa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu ujao.

Hata hivyo, kocha huyo ana mambo saba ambayo anatakiwa kukabiliana nayo ili kuhakikisha kikosi hicho kinafanikiwa kufanya vizuri msimu ujao.

YANG 02

YANGA MPYA

Mtihani wake wa kwanza ni kuunganisha kikosi kipya kwa haraka. Dalili zinaonyesha Yanga inaweza kuwa miongoni mwa timu zitakazobadilisha sura ya kikosi katika dirisha hili, wachezaji kadhaa wa kigeni wanatarajiwa kuwasili huku wengine wakiondoka kutokana na kiwago chao ambacho walikionyesha msimu uliopita.

Prince Dube tayari ameondoka, Pacome Zouzoua hayupo kwenye mipango ya msimu mpya kutokana na kusumbuliwa na majeraha, beki Frank Assinki, Mohamed Damaro, Lassine Kouma na Chadrack Boka nao wamehusishwa na kuondoka kwenye kikosi hicho kabla msimu haujaanza.

Hiyo inamaanisha Manqoba hataanza na kikosi kilichozoeana. Atalazimika kujenga timu yake upya ili kuhakikisha kuwa wachezaji wanazoeana atatakiwa kufanya usajili kabambe, lakini pia kuhakikisha anakaa na timu kwa zaidi ya wiki tatu mazoezini ili kikosi hicho kitakapoanza msimu mambo yawe safi bila visingizio.

YANG 01

HAKUNA MUDA

Kama kuna kitu ambacho Manqoba anatakiwa kukielewa mapema kabisa ni kwamba ameingia katika mazingira ambayo muda ni bidhaa adimu. Soka la Tanzania, hasa katika klabu za Yanga na Simba, halina utamaduni wa kusubiri kocha ajenge timu kwa utulivu. Matokeo ndiyo lugha pekee inayoeleweka.

Mashabiki hawataki kusikia maneno ya ‘mchakato’, ‘kujenga kikosi’ au ‘projekti ya muda mrefu.’ Wanataka kuona timu inashinda kuanzia mchezo wa kwanza, inacheza soka la kuvutia na inaonyesha dalili za kutwaa mataji.

Kushindwa mara mbili au tatu mfululizo kunaweza kugeuza hali ya hewa ndani ya klabu kwa haraka kuliko kocha anavyoweza kubadili mfumo wa uchezaji.

Hiyo ndiyo hali ambayo imewaangusha makocha wengi waliopita akiwemo Roman Folz. Wapo walioingia wakiwa na wasifu mzuri na mafanikio makubwa, lakini hawakupata nafasi ya kutekeleza falsafa zao kwa sababu matokeo ya mwanzo hayakuwa upande wao.

Kwa Manqoba, ugumu unaongezeka zaidi kwa sababu anaingia wakati Yanga inafanya mabadiliko makubwa ya kikosi lakini mchezo wake wa kwanza wa mashindano anacheza na Simba ambao hawajafanikiwa kuifunga Yanga kwa muda mrefu, kama akipoteza mchezo huo wa Ngao, alamu itaanza kulia kichwani.

Ndiyo maana mtihani wake mkubwa hautakuwa tu kufundisha, bali kupata matokeo huku akiwa bado anaijenga timu. Huo ndiyo mzigo ambao makocha wa timu kubwa Afrika huubeba na Manqoba ataukuta Jangwani.

YANG 01

VIWANGO VYA WALIOPOTEA

Ni kweli Yanga ilitwaa ubingwa msimu uliopita, lakini wengi waliona timu haikuwa na ubora ule wa enzi za Miguel Gamondi.

Ile Yanga iliyokuwa inaushambulia mpinzani kwa kasi, inafunga mabao mengi na kutawala mechi kwa dakika 90 haikuonekana mara nyingi na ndiyo maana msimu uliopita ndiyo timu hiyo ilikusanya pointi chache tofauti na ule wa nyuma.

Mashabiki wanataka kuiona timu yao ikirudi katika kiwango hicho, huo ndiyo utakuwa mtihani mwingine wa Manqoba.

Hatatakiwa kushinda pekee, bali kushinda kwa soka ambalo mashabiki watalifurahia kwa kuwa utamaduni wa Yanga ni kuona soka lao wanalotaka na siyo analokuja nalo kocha mpya.

YANG 03

USHINDANI NA SIMBA

Hakuna jambo litakalompima Manqoba haraka kama ushindani dhidi ya Simba, ameingia Yanga katika kipindi ambacho wapinzani wao wa jadi wanaonyesha dalili za kurudi kwenye ubora baada ya misimu minne ya kutafuta mwendelezo.

Chini ya Steve Barker ambaye anafahamiana vyema na Manqoba, Simba imeanza kupata utambulisho mpya, ikarejesha ari ya ushindani na kutwaa Kombe la CRDB Federation pamoja na lile la Muungano baada ya kulisubiri makombe kwa muda mrefu, siyo ishara nzuri kwa Yanga.

Hiyo inaifanya Kariakoo Derby ya msimu ujao kuwa na uzito mkubwa kuliko kawaida. Kwa Yanga, lengo ni kulinda utawala walioujenga kwa misimu ya karibuni na kuthibitisha kuwa bado wao ndiyo nguvu kubwa ya soka la Tanzania. Kwa Simba, huu ni wakati wa kuonyesha kwamba enzi yao imerejea na kwamba mafanikio ya Kombe la CRDB haikuwa bahati mbaya.

Kwa mazingira hayo, kila mchezo kati ya timu hizo mbili hautakuwa wa kutafuta pointi tatu pekee. Utakuwa kipimo cha ubora wa makocha, ubora wa sajili mpya na mwelekeo wa kila timu katika mbio za ubingwa. Mara nyingi matokeo ya Derby ndiyo hujenga au kubomoa imani ya mashabiki kwa kocha, hata kama msimu ukiwa ndio kwanza umeanza.

Presha kwa Manqoba itaongezeka zaidi kwa sababu atalinganishwa moja kwa moja na Barker. Mashabiki na wachambuzi watataka kuona ni kocha gani mwenye mbinu bora, nani anasoma mchezo vizuri zaidi na nani ana uwezo wa kufanya vizuri katika mechi kubwa.

YANG 02

VITA YA MAKOCHA

Mbali na kupigania mataji, Manqoba ataingia pia kwenye vita ya heshima dhidi ya mwenzake kutoka Afrika Kusini, Steve Barker. Kwa mara ya kwanza katika historia ya hivi karibuni ya soka la Tanzania, timu mbili kubwa nchini zinaongozwa na makocha kutoka taifa moja, jambo ambalo linaongeza mvuto na presha ya ushindani wao.

Kwa kawaida, kila mmoja atakuwa na malengo yake ya ndani ya klabu, lakini kwa macho ya mashabiki na wachambuzi, vita hii itakuwa zaidi ya Yanga dhidi ya Simba. Itakuwa pia ni mapambano ya falsafa mbili za ukocha kutoka Afrika Kusini. Kila mmoja atataka kuthibitisha kuwa mbinu zake ndizo bora zaidi na kwamba ndiye kocha mwenye uwezo mkubwa.

Ulinganisho kati yao hauwezi kuepukika. Kila ushindi wa Barker utaibua maswali kuhusu Manqoba na kila ushindi wa Manqoba utaongeza presha kwa Barker. Takwimu zao zitafuatiliwa, rekodi zao zitahesabiwa na kila Derby itachukuliwa kama kipimo cha nani amemzidi mwenzake, kule Afrika Kusini walishakutana na Manqoba anaonekana kuwa bora zaidi, lakini je hali hiyo itakuwa na hapa nchini?

YANG 07

UTAWALA WA YANGA

Kazi kubwa kuliko zote ni kuhakikisha Yanga inaendelea kutesa baada ya kufanya hivyo kwa msimu mitano mfululizo ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, kulinda utawala kwa misimu mfululizo ndiyo kazi inayowatofautisha makocha wakubwa na wa kawaida.

Changamoto ni kwamba anaikuta Yanga ikiwa katika kipindi cha mabadiliko. Baadhi ya nyota walioifanya timu itawale kwa misimu iliyopita wameondoka, wengine wanakaribia kuondoka huku baadhi wakikabiliwa na majeraha na hata  kushuka kwa kiwango. Hivyo, atalazimika kujenga msingi mpya bila kuharibu ushindani ambao tayari umejengwa.

Mwisho wa yote, mafanikio yake hayatapimwa kwa idadi ya sajili mpya wala mfumo wa uchezaji atakaoutumia. Atapimwa kwa uwezo wake wa kuifanya Yanga iendelee kuwa timu ya kuogopwa nchini na barani Afrika. Huo ndio mtihani mkubwa zaidi unaomsubiri Jangwani.

YANG 04

WADAU WASHAURI

Wakiongelea mitihani hiyo inayomsubiri Manqoba, wadau wa soka nchini wametoa maoni tofauti,baba mzazi wa straika wa zamani wa Yanga, Jerry Tegete, Mzee John Tegete amesema presha kubwa itaanzia kwenye Derby.

“Anaweza kuwa na wasifu mkubwa, lakini Tanzania watu watamkumbuka kwa mechi dhidi ya Simba. Akianza vizuri ataaminika mapema, lakini akiteleza mashabiki wataanza kuhoji kila uamuzi wake hapa kuna mtihani sana kwa kuwa pia nafikiri wanakutana mwanzoni kabisa mwa msimu, akishinda hakutakuwa na maswali akipoteza maswali yataanza,”  amesema.

Kwa upande beki wa zamani wa Yanga, Ladisalus Mbogo amesema;”Yanga imepoteza baadhi ya wachezaji waliokuwa uti wa mgongo wa timu. Huwezi kutarajia kocha abadilishe kila kitu ndani ya wiki chache. Kitu muhimu ni kuona timu inaanza kupata mwelekeo na utambulisho wake, kikubwa ni lazima wakubaliane na hali hiyo mwanzoni mwa msimu,” amesema.

Aliyekuwa mchezaji wa Golden Arrows, Knox Mtizwa ambaye aliwahi kufanya kazi chini ya Manqoba huko Afrika Kusini, alimuelezea kocha huyo kwa kusema ni mmoja kati ya makocha bora Afrika.

“Manqoba ni kocha anayependa nidhamu ya kiufundi. Anataka timu yake iwe na mpangilio, kumiliki mpira kwa akili na kushambulia kwa kasi pale nafasi inapopatikana. Anafanya kazi sana kwenye mazoezi ya mbinu na anawafanya wachezaji waelewe majukumu yao kwa undani, sina shida naye sana kama Yanga wataamua kumvumilia mazuri yatakuja,” amesema.

Kwa mujibu wa chanzo cha ndani kutokana Yanga, kocha huyo anatarajiwa kutua nchini hivi karibuni kwa ajili ya kuanza kazi ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi.