Sio poa... Nusu fainali CWC mzigo upo hivi

Muktasari:
- Katika mechi za robo fainali kulikuwa na matukio mbalimbali na moja kati ya matukio yaliyosikitisha zaidi ilikuwa ni majeraha aliyopata mshambuliaji wa Bayern Munich, Jaml Musiala katika mchezo kati ya timu yake na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG.
NEW YORK, MAREKANI: HATUA ya robo fainali za Kombe la Dunia la Klabu la FIFA ilimalizika jana ambapo timu nne zimefuzu kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.
Katika mechi za robo fainali kulikuwa na matukio mbalimbali na moja kati ya matukio yaliyosikitisha zaidi ilikuwa ni majeraha aliyopata mshambuliaji wa Bayern Munich, Jaml Musiala katika mchezo kati ya timu yake na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG.
Musiala ambaye amepata jeraha baya la mguu baada ya kugongana na kipa wa PSG, Gianluig Donnarumma anakadiriwa kuwa atakuwa nje kwa miezi kati ya minne hadi mitano.
Donnarumma mwenyewe alionekana akimwaga machozi baada ya kugongana na Musiala na baadaye akaomba msamaha kupitia mitandao ya kijamii, hata hivyo kipa wa Bayern Manuel Neuer alimlaumu na kusema hakutakiwa kucheza vile.
“Ilikuwa ni hatari sana kucheza vile, ilionekana kama alijiandaa kwa matokeo ya namna alivyocheza. Mimi binafsi nisingeingia vile.”
Mbali ya tukio hili ambalo lilitokea kwenye mechi hii ya PSG na Bayern iliyomalizika kwa PSG kushinda mabao 2-0, pia kulikuwa na matukio mbalimbali yaliyojiri katika mechi ya jana.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa PSG kushiriki michuano hii na kufanikiwa kufika hatua hiyo ambapo mchezo wa nusu itakutana Real Madrid ambao ndio mabingwa wa kihistoria wa michuano hii wakiwa wamechukua taji hili mara nyingi zaidi (5) kati ya mara sita walizoshiriki.
Madrid ilifuzu hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Borussia Dortmund mabao 3-2 ambayo yalifungwa na Garcia Torres, Francisco Garcia na Kylian Mbappe wakati yale ya Dortmund yakifungwa na Serhou Guirassy na Maximilian Beier.
Katika mchezo huu, Mbappe na Trent Alexander Arnold walionekana kutuma salamu kuonyesha kuguswa kwao na kifo cha Diogo Jota ambapo Mbappe baada ya kufunga alionyesha ishara ya jezi ya Jota wakati Trent akionekana anaangusha machozi wakati timu zimesimama kabla ya mechi kwa ajili ya kuomboleza kifo cha staa huyo.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Dortmund kucheza michuano hii na kocha wao Niko Kovac baada ya kupoteza mchezo amekosoa viwanja vinavyochezewa mechi hizo akisema vina hadhi ya kuandaa mechi za gofu na sio mpira wa miguu.
Nusu fainali ya kwanza kati ya Madrid na PSG inatarajiwa kupigwa Julai 9, kuanzia saa 4:00 usiku katika dimba la Metlife.
Madrid ambayo imeshiriki mara sita michuano hii, imewahi kuishia mara moja tu nusu fainali ambayo ilikuwa ni mwaka wa kwanza 2000 wa michuano hii kwa mfumo mpya ambapo ilimaliza mshindi wa nne baada ya kupoteza mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Necaxa ya Mexico kwa penalti 4-3.
Nusu fainali nyingine itakuwa ni kati ya Fluminense na Chelsea. Fluminense ilifika hatua hiyo baada ya kuichapa Al-Hilal ya Saudi Arabia kwa mabao 2-1.
Vilevile Chelsea ilifuzu kwa kuichapa Palmeiras mabao 2-1 katika mechi ambayo ilishindikana kwa Palmeiras kulipa kisasi na ikapokea kichapo kwa mara ya pili.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa ni mwaka 2022 katika fainali ya michuano hii ambapo Chelsea ilishinda mabao 2-1.
Mchezo kati ya Fluminense na Chelsea utakaopigwa katika dimba la Metlife kesho kuanzia saa 4:00 usiku pia utakuwa wa kwanza kwa timu hizo kukutana.
Hii ni mara ya tatu kwa Chelsea kufika nusu fainali ya michuano hii, mara mbili za nyuma ilizowahi kufika hatua hiyo ilifika fainali.