Simu yamponza Depay, mwenyewe afafanua
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi alieleza sababu ya kutumia simu alipokuwa amekaa benchi, alikuwa akifanya mawasiliano na matabibu wake waliopo nchini kwao.
SAO PAOLO, BRAZIL: STRAIKA wa Corinthians ya Brazil, Memphis Depay amelazimika kutoa ufafanuzi baada ya kuonekana akitumia simu akiwa benchi baada ya kuambiwa aache kufanya hivyo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi alieleza sababu ya kutumia simu alipokuwa amekaa benchi, alikuwa akifanya mawasiliano na matabibu wake waliopo nchini kwao.
Inaelezwa alikemewa na mmoja wa makocha wa timu hiyo wakati wa sare juzi dhidi ya Flamengo katika mchezo wa Ligi Kuu ambao nyota huyo alionekana akitumia simu katika muda wa nyongeza mwishoni mwa kipindi cha pili, akiwa amekaa pamoja na wachezaji wenzake.
Awali, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alitolewa uwanjani mapema katika dakika ya 22 kutokana na jeraha katika mchezo wa Campeonato Brasileiro Série A.
Kadri mchezo ulivyokuwa ukielekea mwisho, kamera za televisheni zilimuonyesha Depay akitumia simu kabla ya kufuatwa na kocha wa Corinthians na inaonekana aliambiwa aache, na baada ya mazungumzo mafupi aliiweka mfukoni.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Depay alifafanua tukio hilo akisema: “Naomba kufafanua, muda wangu na simu ulikuwa kwa ajili ya kuwasiliana na madaktari wangu nchini Uholanzi wakati huo. Nilitoka nje kuipa timu yangu sapoti wakati ningeweza kubaki chumba cha kubadilishia nguo kutokana na jeraha.
“Pia nimeumizwa na matokeo ya mchezo. Tunaendelea kufanya kazi kwa siku bora zijazo.”
Depay pia ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uholanzi kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Norway na Ecuador, ingawa ukubwa wa jeraha lake bado haujajulikana. Mchezo huo uliisha kwa sare ya 1-1, ambapo Lucas Paqueta aliifungia Flamengo bao la kwanza kabla ya Yuri Alberto kuisawazishia Corinthians.
Licha ya wapinzani wao kubaki na wachezaji 10 kipindi cha pili, Corinthians walishindwa kupata bao la ushindi.
Matokeo hayo yanaiacha Corinthians nafasi ya 11 kwenye msimamo baada ya mechi nane, huku Flamengo wakiwa nafasi ya nne, tofauti ya pointi nne.