Zidane kulamba dili jipya Ufaransa
Muktasari:
- Akiwa kocha wa Ufaransa, Deschamps ana rekodi ya kuvutia ya ushindi mara 113, sare 32 na vipigo 30 katika mechi 175. Mafanikio hayo makubwa yana maana Zidane ikiwa atateuliwa atakuwa na kazi ngumu ya kuthibitisha.
MADRID, HISPANIA: KOCHA na mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Zinedine Zidane anatarajia kupata kazi mpya baada ya kufikia makubaliano ya mdomo ili kumaliza siku 1,727 za bila ajira.
Kwa mujibu wa gazeti la Ufaransa, Le Parisien, Zidane anajiandaa kurejea katika ukocha ili kuiongoza timu ya taifa ya nchi hiyo na taarifa zinadai tayari amefikia makubaliano ya mdomo na Shirikisho la Soka Ufaransa (FFF) ili kumrithi kocha wa sasa, Didier Deschamps, baada ya fainali za Kombe la Dunia 2026.
Habari za makubaliano hayo zinakuja muda mfupi baada ya Rais wa FFF, Philippe Diallo, kuthibitisha tayari amechagua mrithi wa Deschamps.
“Ndiyo, najua nani atakuwa kocha ajaye wa Ufaransa.”
Tangu Januari, mwaka jana, Deschamps alifunguka juu ya kuachia nafasi hiyo baada ya fainali hizo. “Nimekuwa hapa tangu 2012, na mkataba wangu unaisha 2026, Kombe la Dunia lijalo. Hapo ndipo nitasimama, kwa sababu lazima ifike mwisho wakati fulani. Kichwani mwangu hilo liko wazi.”
Aliongeza, “Nimetimiza wajibu wangu kwa hamasa ileile ya kuhakikisha timu ya Ufaransa inabaki juu. Hatutaki kitu kizuri kiishe, lakini lazima ujue wakati wa kusema basi. Kuna maisha baada ya hili. Sijui yatakuwaje, lakini yatakuwa mazuri pia.”
Deschamps alisisitiza, “itakuwa miaka 14. Ni muda mrefu sana. Sipo hapa kwa ajili ya rekodi, bali kuhakikisha timu ya Ufaransa inaendelea kuwa kileleni.”
Deschamps amekuwa na mafanikio makubwa akiwa kocha wa Ufaransa akiiongoza kushinda Kombe la Dunia 2018 na kukaribia kutetea taji hilo 2022, jambo ambalo lingekuwa la kwanza tangu Brazil ilipofanya hivyo 1962, lakini ilipoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Argentina.
Akiwa kocha wa Ufaransa, Deschamps ana rekodi ya kuvutia ya ushindi mara 113, sare 32 na vipigo 30 katika mechi 175. Mafanikio hayo makubwa yana maana Zidane ikiwa atateuliwa atakuwa na kazi ngumu ya kuthibitisha.