Simba pasi mbili bao

ILE siku ya hukumu inazidi kukaribia kabla ya kikosi cha Simba kuvaana na Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini huko mazoezini, kocha Didier Gomes ameonekana kukomaa na washambuliaji wake akiwataka kutumia nafasi za kufunga kwa pasi mbili tu ikiwa ni mbinu za kutaka kuimaliza Yanga.

Kocha huyo Mfaransa kwenye mazoezi juzi Jumanne, alionekana kuwapa maelekezo maalumu nyota wake wanne wanaocheza eneo la ushambuliaji, akitaka kutopoteza nafasi wanazopata kwa pasi moja, mbili kisha wanatupia kambani, jambo linaloweza kuwapa wakati mgumu mabeki wa Jangwani.

Katika mazoezi hayo ya muda usiopungua saa mbili yakianza saa 10:30 jioni, wachezaji wa Simba walifanya ya aina mbalimbali ikiwemo yale ya viungo, yaliyosimamiwa na Adel Zrane pamoja na yale ya kiufundi yaliyosimamiwa na Gomes akisaidiana na Seleman Matola.

Gomes katika zoezi hilo la kufunga aliwakomalia na kuwapa mbinu Chriss Mugalu, Meddie Kagere, John Bocco na Bernard Morrison ambaye alionyesha kiwango bora pengine kuliko wachezaji wote siku hiyo.

Katika zoezi hilo, Gomes aliwataka viungo wake Clatous Chama, Larry Bwalya na Luis Miquissone kuwatengenezea nafasi za kufunga, Mugalu, Kagere, Bocco na Morrison waliokuwa wakikabwa na Ibrahim Ame, Erasto Nyoni na Pascal Wawa ambao walifanya yao na kuwapa burudani mashabiki.

Mwanaspoti, lililoweka kambi kwa muda kwenye mazoezi hayo, lilishuhudia kuna wakati Ame, Nyoni na Wawa walifanikiwa kuwakaba lakini muda mwingi, makipa Benno Kakolanya, Aishi Manula na Ally Salim waliishia kutunguliwa mabao na mastraika hao na kumfurahisha Gomes.

Katika zoezi hili la kufunga, Morrison alionyesha kuitaka mechi na Yanga kwani alikuwa moto kwa kuonyesha kiwango bora kwenye kufunga, alifunga mabao saba, alipora mipira, alitengeneza nafasi za kufunga kwa Mugalu, Kagere na Bocco.

Morrison hakuishia hapo alikuwa mchezaji ambaye anazunguka katika maeneo mengi kusaka mipira ili kutimiza majukumu hayo, wakati huo huo katika zoezi hilo, Mugalu alifunga mabao matano, Bocco na Kagere kila mmoja alifunga manne.

Katika zoezi hilo Gomes alionekana kuwa mkali kwani alitaka kuona viungo wanapiga pasi sahihi na kutengeneza nafasi za kufunga huku Mugalu, Kagere, Bocco na Morrison walitakiwa kuwa na uharaka kutogusa mpira zaidi ya mara tatu na kufunga bao.

Wakati Morrison akiwa ameng’aa, mastraika hao watatu Mugalu, Kagere na Bocco nao walicheza kwa kuelewana kutengenezena nafasi za kufunga na muda mwingine kujirahisishia kazi hiyo.

Kutokana na aina hiyo ya mazoezi mabeki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Dickson Job, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Kibwana Shomary na Adeyun Saleh watakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia washambuliaji hao.


MSIKIE GOMES

Kocha wa Simba, Gomes alisema wakati huu wanafanya yale yote ambayo alikuwa anawaelekeza wachezaji wake kutokana na vile ambavyo waliviona kutoka kwa wapinzani wao ili kwenda kufanya vizuri katika mechi hiyo.

“Baada ya kuona vitu vya kiufundi niliwalekeza wachezaji wangu kwa nadharia ila wakati huu ndio tunavifanya kwa vitendo ili kuhakikisha tunawazidi kutokana na udhaifu wao na pia kuwazuia kutokana na ubora wao,” alisema Gomes, huku winga Mghana, Morrison alisisitiza wanaendelea kufanya maandalizi ya kutosha ili kuendeleza ubora wa kupata matokeo mazuri ambao walikuwa nao tangu awali katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara.

“Mara nyingi mechi za namna hii zinakuwa na ushindani wa kutosha ila kwa upande wetu tunaendelea na maandalizi ya msingi kulingana na wapinzani wetu walivyo ili kuwazidi na kupata matokeo,” alisema winga huyo aliyetokea Yanga.