Safari ya Mwisho ya Baba wa Mbwana Samatta

Muktasari:
- Akizungumza kwa majonzi, Rajabu Samatta mtoto wa kwanza wa marehemu, amesema, Mzee Samatta alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya presha pamoja na kisukari, hali ambayo ilizidi kudhoofisha afya yake katika siku za hivi karibuni.
FAMILIA ya straika nyota na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta ipo katika majonzi makubwa kufuatia kifo cha baba yao mpendwa, Mzee Ally Samatta, aliyefariki dunia leo Jumapili baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akizungumza kwa majonzi, Rajabu Samatta mtoto wa kwanza wa marehemu, amesema, Mzee Samatta alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya presha pamoja na kisukari, hali ambayo ilizidi kudhoofisha afya yake katika siku za hivi karibuni.
"Tumehangaika naye kwa madaktari kwa muda mrefu. Kuna wakati sukari ilikuwa inakaa sawa, lakini baadaye inabadilika ghafla,” amesema.
Rajabu amesema, pamoja na ushauri wa madaktari na familia kutomruhusu kusafiri, Mzee Ally aliendelea kushikilia desturi yake ya kwenda kaburini kwa mke wake kila mwezi wa sita kwa ajili ya kuswali, kuomba dua, na kusafisha kaburi hilo jambo ambalo mwaka huu lilizidisha hali yake kiafya.
“Tulimwambia sana mzee asisafiri masafa marefu, lakini alikuwa na desturi hiyo ya kwenda kumtembelea mama kaburini Juni ya kila mwaka, safari hiyo ya mwaka huu ndio ilizidisha hali yake," amesema Rajabu na kuongeza; "Baada ya kukaa kwenye gari muda mrefu, miguu yake ilianza kushindwa kufanya kazi, kama imeparalaizi."
Mzee Ally alirudishwa hospitali ya Polisi kwa uangalizi ambapo madaktari walibaini kuwa kiwango cha sukari kilikuwa juu mno, hadi kufikia karibu 20 hali iliyomuweka hatarini. Baada ya vipimo, aliruhusiwa kurudi nyumbani akiwa kwenye uangalizi wa karibu huku akiendelea kutumia dawa.
“Alikuwa na hasira kipindi anaumwa. Alikataa kula, akisema hana hamu atakula. Tulikuwa tukimpigia simu kila mara mimi nikiwa Mbeya,” amefafanua Rajabu.
Kwa mujibu wa Rajabu, hali ya baba yao ilibadilika ghafla Jumatano ambapo waliamua kumpeleka tena hospitali ya Polisi. Madaktari walishauri apelekwe Muhimbili kwa matibabu zaidi, lakini kabla ya hatua hiyo kutekelezwa, mauti yalikuwa yamemfika.
“Bahati mbaya tulimpoteza jana. Mwili wake kwa sasa upo hospitali ya Polisi, tutaenda kuuchukua kesho (Jumatatu) saa nne asubuhi na kuuleta hapa (Mbagala) kwa ajili ya kusomewa dua. Saa sita tutaanza safari ya kwenda Kibiti kwa mazishi.”
Kwa mujibu wa Rajabu, marehemu Mzee Ally Samatta alikuwa amewahi kueleza kuwa akifariki dunia angependa azikwe eneo la Kibiti ambapo pia ndipo alipozikwa baba yake mzazi.
Kifo cha Mzee Samatta kimeacha pengo kubwa sio tu kwa familia bali pia kwa jamii iliyomfahamu kama mzee mwenye hekima, mpenda familia na mwenye kushikilia mila na desturi. Ameacha watoto kadhaa wakiwemo Mbwana Samatta, ambaye ni nembo ya soka la Tanzania.
Rambirambi zinaendelea kumiminika kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo, ndugu, jamaa na marafiki.
Gazeti la Mwanaspoti linatoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa Samatta na wadau wa soka kwa ujumla.