Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simanzi, kocha afariki kwenye mechi

Muktasari:

  • Taifa hilo limekumbwa na huzuni kubwa wikiendi iliyopita baada ya kocha wa timu ya Radnicki 1923, Mladen Zizovic kuanguka uwanjani wakati akiitazama timu yake ikipambana na Mladost.

BELGRADE, SERBIA: MASTAA wa timu moja ya soka huko Serbia hawakuwa na namna zaidi ya kuangua tu vilio na wengine wakilala kwenye nyasi za uwanja baada ya kupewa taarifa kocha wao amefariki dunia wakati mchezo wa ligi ya juu ya nchi hiyo ukiwa unaendelea.

Taifa hilo limekumbwa na huzuni kubwa wikiendi iliyopita baada ya kocha wa timu ya Radnicki 1923, Mladen Zizovic kuanguka uwanjani wakati akiitazama timu yake ikipambana na Mladost.

Ilikuwa dakika ya 22 ya mchezo huo uliofanyika Jumapili, kocha huyo alipatwa na shambulio la moyo na kuanguka, kiasi cha kuwafanya madaktari kuwahi kumpa huduma ya dharura. Mechi ilisimama kumpisha kocha huyo, Zizovic kupatiwa huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa hospitalini.

Baadaye mwamuzi aliamuru mchezo kuendelea, lakini dakika 20 baadaye, zililetwa taarifa uwanjani hapo zilizothibitisha kwamba kocha huyo amefariki dunia wakati akiwa njiani kupelekwa hospitali. Jambo hilo liliibua mshtuko mkubwa kwa wachezaji wa timu zote mbili, huku wengine wakiishiwa nguvu na kulala kwenye nyasi za uwanja na wengine wakimwaga machozi huku wakipiga magoti kama kutoa heshima kwa kocha huyo.

Uwanja mzima uligubikwa na ukimya mkubwa baada ya taarifa hizo. Klabu ya Radnicki baadaye ilitoa taarifa iliyosomeka: “Ni maumivu makubwa na hatuamini” ikielezea kifo cha Zizovic.

Taarifa hiyo iliendelea: “Mtu ambaye ameacha alama kila mahali alipofanya kazi kutokana na maarifa yake, utulivu na uwezo. Ingawa amekuwa na kipindi kifupi Kragujevac, ameweza kujijengea heshima kwa kila mtu kwenye klabu, wachezaji, mashabiki kutokana na weledi wake na utu. FK Radnicki 1923 imetuma salamu za pole kwa familia, marafiki na kila mtu aliyemfahamu Mladen.

“Kujitolea kwake kwenye soka, upendo kwenye mchezo na utu wake utabaki kwenye kumbukumbu zetu milele, ni heshima kubwa kwetu kumfahamu. Pumzika kwa amani, Mladen.”€

Wakati huo huo, kuna mchezaji mmoja alifichua kwamba Zizovic alilalamikia mlo wake wa samaki saa kadhaa kabla ya kukumbwa na shambulio hilo la moyo.

Mehmed Cosic aliambia Faktor: “Sikulala hadi saa 9:30 alfajiri. Nimeishiwa maneno, sote tumeduwaa. Wanasema, alilalamika kuhusu samaki, alisema hatakula tena. Hicho ndicho alichokuwa akisema. Hakukuwa na tatizo wakati wa kupasha misuli moto, mechi ilianza na kila kitu kilionekana kipo sawa.”

Zizovic, ambaye ni staa wa zamani wa kimataifa wa Bosnia alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo, Oktoba 23. Mechi hiyo dhidi ya Mladost ulikuwa mchezo wake wa tatu tangu alipokabidhiwa mikoba hiyo ya ukocha kwenye timu hiyo na hivyo kuacha huzuni kubwa Serbia.

Chama cha soka Serbia kilisema: “Chama cha soka Serbia kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha kocha wa FK Radnički 1923, Mladen Zizovic, aliyefariki dunia katika mechi ya Mozzart Bet Super League ya Serbia kati ya Mladost na Radnicki 1923 mjini Lucani.

“Kifo chake ni pigo kubwa kwa jamii ya soka. Apumzike kwa amani, Mladen. Mapenzi yako ya soka yatabaki kwenye mioyo yetu milele.”

Miamba ya soka ya Serbia, Partizan Belgrade kwenye taarifa yake iliongeza: “Ni huzuni kubwa, tumepokea taarifa za kifo cha kocha wa Radnicki kutoka Kragujevac, Mladen Zizovic, amefariki ghafla."