Siku 19 baada ya ajali, AJ atangaza kurudi ulingoni
Muktasari:
- Joshua maarufu AJ alirejea mazoezini takriban wiki mbili zilizopita ikiwa ni siku chache tangu alipopata ajali ya gari ya huko Nigeria iliyosababisha vifo vya marafiki zake wawili wa karibu ambao pia walikuwa wasaidizi wake ulingoni.
LONDON, ENGLAND: BONDIA wa ngumi za uzito wa juu duniani kutoka England, Anthony Joshua amepanga kurejea ulingoni kuzichapa katika mchezo utakaochezwa wakati wowote mwaka huu, ingawa hadi sasa haijafahamika kambi yake inazungumza na mabondia gani.
Joshua maarufu AJ alirejea mazoezini takriban wiki mbili zilizopita ikiwa ni siku chache tangu alipopata ajali ya gari ya huko Nigeria iliyosababisha vifo vya marafiki zake wawili wa karibu ambao pia walikuwa wasaidizi wake ulingoni.
Bingwa huyo wa zamani wa dunia wa uzani wa juu mwenye umri wa miaka 36 alipata majeraha madogo katika ajali hiyo iliyotokea Nigeria Desemba 29, mwaka jana, iliyosababishwa na mwendo kasi wa gari walilokuwa wakisafiria kwenda kijijini na eneo la asili la bondia huyo huko Ogun.
Katika ajali hiyo Sina Ghami na Latif ‘Latz’ Ayodele walifariki dunia papo hapo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali ambamo Joshua pia alikuwa abiria. Gari walilokuwamo liligonga lori lililokuwa limesimama kando ya barabara kwenye barabara kuu karibu na Lagos.
Siku 19 baada ya ajali hiyo, Joshua aliweka video kwenye Snapchat ikimuonyesha akifanya mazoezi ya kupiga ‘pad’ na kufanya mazoezi ya viungo, ikiwa na ujumbe ‘tiba ya nguvu ya akili’ chini ya moja ya ‘clip’.
Joshua alimchapa Jake Paul mjini Miami, Marekani, Desemba 19 siku 10 kabla ya ajali hiyo kutokea akiwa likizo.
Wiki iliyopita aliweka ujumbe wa kumbukumbu kumuenzi kocha wake wa fiziki na mazoezi, Ghami pamoja na mkufunzi wake Ayodele kupitia Instagram kisha aliandika: “Sikuwahi hata kutambua jinsi walivyokuwa watu wa kipekee.
“Nilikuwa natembea nao tu na kupiga nao stori bila hata kujua Mungu alikuwa amenifanya niwe karibu na watu bora kiasi kile. Kwa asilimia 100 ni jambo gumu kwangu kulikubali, lakini najua ni gumu zaidi kwa wazazi wao.”
Promota wa Joshua, Eddie Hearn anaamini kuwa Joshua atarejea kwenye ndondi ‘wakati utakapokuwa sahihi’€ na akizungumza na Sky Sports, amesema: “Atahitaji muda kwa ajili ya kupata tiba ya kimwili, kiakili, kihisia na kiroho kabla ya kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake. Ninaamini atataka kurejea kwenye ndondi, lakini huo utakuwa uamuzi wake mwenyewe, wakati utakapokuwa sahihi.”
Amesema: “Hakika sitakuwa na mazungumzo naye kwa sasa. Mazungumzo pekee ni ‘je, uko sawa?’ na wakati mwingine watu huonyesha sura ya kuwa wako sawa, lakini kilichomtokea si jambo la kawaida na ni la kuhuzunisha kwa wote walioguswa.
“Wakati utakapokuwa sahihi, naamini atafanya uamuzi wake na mtasikia moja kwa moja kutoka kwake. Hiyo ndiyo sauti pekee mnayopaswa kuisikiliza katika suala hilo, na tutampa muda wa kupona na kupona majeraha yake.”€
Hata hivyo, kwa kile kinachoendelea mazoezini kwake inaelezwa kwamba ni kama ameshapanga mwaka huu hauwezi kupita bila kuzichapa ikizingatiwa kwamba licha ya kuwa hufanya mazoezi ya kawaida kila mara, lakini kwa wanaomjua anapotaka kuzichapa au kuandaa pambano, hupiga tizi mara mbili au tatu kwa siku.
“Hicho ndicho kinachoendelea katika mazoezi yake. Huyu mtu anafanya mazoezi kwa sasa kana kwamba ni kesho au keshokutwa anazichapa na mpinzani wake yupo tayari. Ni suala la kusubiri tu muda utaongea,” kilisema chanzo kutoka ndani ya kambi yake.