Joshua aanza tizi, kuhusu kustaafu sikia hii
Muktasari:
- Bingwa huyo wa zamani wa uzito wa juu, 36, alipata majeraha madogo mwishoni mwa Desemba, baada ya gari aina ya Lexus SUV alilokuwa akisafiria kugongana na lori lililokuwa limesimama kwenye barabara kuu karibu na Lagos, Nigeria.
LONDON, ENGLAND: BAADA ya tetesi zilizodai anaweza akastaafu, Bondia raia wa England, Anthony Joshua amechapisha kwa mara ya kwanza video za mazoezi yake tangu apate ajali mbaya ya gari iliyosababisha vifo vya marafiki zake wawili wa karibu.
Bingwa huyo wa zamani wa uzito wa juu, 36, alipata majeraha madogo mwishoni mwa Desemba, baada ya gari aina ya Lexus SUV alilokuwa akisafiria kugongana na lori lililokuwa limesimama kwenye barabara kuu karibu na Lagos, Nigeria.
Marafiki zake wa karibu, Sina Ghami na Latif ‘Latz’ Ayodele, walifariki dunia hali iliyoibua masikitiko makubwa.
Baada ya kukaa kwa muda mfupi hospitalini, Joshua alirejea England na kuhudhuria mazishi ya Ghami na Ayodele yaliyofanyika katika msikiti mmoja jijini London Januari 04.
Wiki iliyopita, Joshua aliwapa heshima marafiki hao wawili, akisema anapata ugumu kukubali ni kweli wamefariki dunia.
"Asanteni kwa upendo na huruma mliyowaonyesha ndugu zangu. Kwa asilimia 100 ni jambo gumu kwangu, lakini najua ni gumu zaidi kwa wazazi wao. Nipo imara kisaikolojia na naamini Mungu anajua mioyo yao. Mungu awarehemu ndugu zangu," amesema Joshua katika ukurasa wake wa Instagram.
Kumekuwa na tetesi kuhusu iwapo Joshua ataamua kustaafu ndondi baada ya tukio hilo la kusikitisha.
Sasa, Joshua amechapisha video kwenye Snapchat ikimuonyesha akifanya mazoezi ya kupiga ngumi, mazoezi ya viungo na kuendesha baiskeli ya mazoezi, huku akiandika ujumbe unaosema “tiba ya nguvu ya akili”.
Kwa mujibu wa promota wake Eddie Hearn, bado hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kuhusu mustakabali wa Joshua. Hearn aliulizwa hivi karibuni kama bondia huyo atachukua mapumziko ya muda mrefu na akasema: "Anahitaji kupumzika ili kuwa sawa kimwili, kiakili, kihisia na kiroho kabla ya kufanya uamuzi kuhusu maisha yake ya baadaye."
"Ninaamini atataka kurejea kwenye ndondi, lakini huo utakuwa uamuzi wake mwenyewe pale atakapokuwa tayari. Kwa sasa, si mazungumzo nitakayokuwa nikifanya naye. Mazungumzo pekee ni, ‘uko sawa?’. Alichopitia si cha kawaida na ni cha kuhuzunisha kwa kila aliyekisikia au kuona."
"Wakati utakapofika, naamini atafanya uamuzi wake na mtausikia kutoka kwake mwenyewe."