Shearer aweka tiki Kane kutua Anfield

Muktasari:
- Liverpool imeelezwa kwamba ichangamkie fursa ya kumchukua Kane endapo kama mshambuliaji huyo atafungua milango ya kutaka kurudi kwenye Ligi Kuu England kwenda kumalizia kiporo chake cha kuvunja rekodi ya mabao.
MUNICH, UJERUMANI: GWIJI, Alan Shearer amesema Liverpool haitaonekana kwamba imetumia akili mbovu endapo itapambana kunasa huduma ya straika wa Bayern Mnnich, Harry Kane kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi huko Ulaya.
Liverpool imeelezwa kwamba ichangamkie fursa ya kumchukua Kane endapo kama mshambuliaji huyo atafungua milango ya kutaka kurudi kwenye Ligi Kuu England kwenda kumalizia kiporo chake cha kuvunja rekodi ya mabao.
Kane, 31, alijiunga na Bayern Munich akitokea Tottenham ikiwa ni mpango wake wa kusaka mataji. Na baada ya kutoka kapa mwaka msimu uliopita, Kane na Bayern yake amejiweka kwenye nafasi nzuri ya kubeba Bundesliga msimu huu.
Kinachoelezwa ni kwamba endapo Kane atafanikiwa kubeba taji msimu huu, basi bila ya shaka atafungua milango ya kurudi England kwenda kuvunja rekodi ya mabao kwenye Ligi Kuu England.
Na hilo limeibuka baada ya kudaiwa kwenye mkataba wa straika huyo kuna kipengele kinachomruhusu kunaswa na timu nyingine kwa ada isiyozidi Pauni 60 milioni kwenye dirisha lijalo na hilo limefanya Liverpool ianze kuhusishwa naye.
Kama Kane atarudi England atakuwa kwenye nafasi kubwa ya kuvunja rekodi ya mabao ya Shearer, aliyefunga mara nyingi kuliko wote kwenye Ligi Kuu England baada ya kutikisa nyavu mara 260.
Na Shearer wala hana hofu ya kupoteza rekodi yake baada ya kusema: “Liverpool itahitaji mshambuliaji wa kati kwenye dirisha lijalo, sina shaka Harry Kane atakuwa chaguo lao bora kutokana na ukubwa wa klabu yao na uwezo wa kufunga wa mchezaji huyo.”
Kama Harry atachagua kubaki Ujerumani au akirudi Ligi Kuu England, hilo ni yeye. Siku zote nimekuwa nikisema kama atarudi Ligi Kuu England atakuwa na nafasi ya kuvunja rekodi yangu. Namkubali sana.”
Kama Kane ataamua kurudi England, Liverpool itakuwa kwenye uhitaji wa Namba 9 mpya baada ya Darwin Nunez kutokuwa na maajabu mbele ya goli.
Liverpool ya kocha Arne Slot ipo kwenye wakati mzuri wa kunyakua taji la Ligi Kuu England msimu huu na uhamisho wa Kane kwenye timu hiyo ya Anfield ukitimia unamweka mchezaji huyo kwenye nafasi ya kunyakua mataji zaidi.