Shangwe la Spurs ilipobeba Europa League

Muktasari:
- Mashabiki wa Spurs hakuwa na namna ya kufurahia kitendo cha kumaliza ukame wa miaka 17 wa kubeba taji baada ya ushindi 1-0, shukrani kwa bao la Brennan Johnson katika fainali hiyo.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa Tottenham Hotspur hakuna walichoona kinatosha zaidi ya kuvamia kwenye uwanja wao kwa furaha baada ya kikosi chao kufanikiwa kunyakua ubingwa wa Europa League kwa kuichapa Manchester United kwenye mchezo wa fainali uliofanyika uwanjani San Mames, Bilbao, Hispania usiku wa Jumatano.
Mashabiki wa Spurs hakuwa na namna ya kufurahia kitendo cha kumaliza ukame wa miaka 17 wa kubeba taji baada ya ushindi 1-0, shukrani kwa bao la Brennan Johnson katika fainali hiyo.
Zaidi ya mashabiki 40,000 wa Spurs ambao walishindwa kusafiri kwenda Hispania ilikofanyika fainali hiyo, waliwekewa skrini kubwa ya televisheni kwenye Uwanja wa Tottenham huko London, England.
Baada ya dakika 90 na mechi kumalizika kwa Spurs kushinda 1-0, hapo ndipo balaa lilipoanza kwa mashabiki wa timu hiyo kupagawa kwa shangwe.

Mashabiki hao wa Spurs walikuwa kwenye furaha ya mambo mawili, kwanza kumaliza ukame wa miaka 17 ya kubeba taji, lakini pili ni kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwa furaha hiyo, mashabiki hao walivuka vizingiti vyote uwanjani Tottenham, huku wengine wakipanda juu ya televisheni hiyo kubwa, wakivua mashati yao na kuyapepea juu.
Na mashabiki wengine walivamia mitaani wakiwa na miale ya moto na kuimba nyimbo ‘London Kaskazini ni yetu!’
Katika mechi hiyo, Man United ilimiliki mpira kwa muda mrefu, lakini hakukuwa na nafasi nyingi za wazi za kufunga huku fainali hiyo iliyokutanisha timu mbili zenye msimu mbaya kwenye Ligi Kuu England kufanya fainali hiyo isiwe tamu sana.
Huko Bilbao, uwanjani watu walijaa na maelfu ya mashabiki walikuwa wakipeperusha bendera na kuimba nyimbo za kutamba.

Shabiki mmoja aliandika kwenye mtandao wa kijamii, akisema: “Nimevunjika, lakini sijali. Tulichohitaji ni kushinda.”
Ushindi huo pia umemfanya kocha Ange Postecoglou kuwa na uhakika wa kuendelea kubaki kwenye kikosi cha Spurs kwa sababu kimekamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kama ilivyokuwa London, huko Hispania nako mitaa ilipambana moto wakati mashabiki 70,000 walipokuwa kwenye shangwe kubwa. Ushindi huo uliipa Spurs ubingwa wa kwanza wa Ulaya tangu mwaka 1984.
Sambamba na tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, Spurs imewekwa kibindoni pia Pauni 100 milioni. Kuna wachezaji watatu walilazimika kusubiri medali zao za ubingwa huo.

Kocha Ange Postecoglou alikuwa wa kwanza kuvalishwa medali na rais wa Uefa, Aleksander Ceferin. Waliokosa medali ni Son Heung-min, Cristian Romero na Rodrigo Bentancur na hivyo kulazimika kusubiri hadi walipoingia vyumbani kupewa medali zao. Kwa mujibu wa sheria za Uefa, timu iliyoshinda na iliyoshindwa kila moja itapewa medali 50.
Uefa iliipa medali 30 baada ya kubeba taji kwa mara ya kwanza kwa miaka 17.