Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa mziki huu, Simba itapindua meza Zanzibar

MZIKI Pict

Muktasari:

  • Marudiano ya mechi hiyo ni Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambapo anachokifanya kocha wa Simba, Fadlu Davids hivi sasa ni kuumiza kichwa ni namna gani apange kikosi kitakachobadili matokeo hayo na kubeba ubingwa.

SIMBA ina deni la mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane lililotokana na kupoteza mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa Jumamosi iliyopita mjini Berkane, Morocco.

Marudiano ya mechi hiyo ni Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambapo anachokifanya kocha wa Simba, Fadlu Davids hivi sasa ni kuumiza kichwa ni namna gani apange kikosi kitakachobadili matokeo hayo na kubeba ubingwa.

Hivi sasa Fadlu anatafuta dawa ya kutibu makosa yaliyofanyika mechi ya kwanza, kwani wakati Simba ikipoteza ugenini, rekodi zinaonyesha timu hiyo haikuwa vizuri kwa kila kitu kuanzia ulinzi hadi ushambuliaji.

Takwimu za mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Simba ilipiga mashuti tisa pekee huku kukiwa hakuna hata moja lililolenga lango, wakati wenyeji wakipiga 14, sita yakilenga lango yaliyozaa mabao mawili.

Pia umiliki wa mpira Simba ilikuwa na asilimia 47 dhidi ya 53 za Berkane wakati pasi za Simba zikiwa 358, Berkane ikipiga 381. Kitu pekee ambacho Simba iliongoza ni kwa kuotea ikifanya hivyo mara mbili, Berkane ni moja, lakini upande wa kona, Berkane ilipiga saba huku moja ikiitumia kufunga bao la kwanza. Simba ilipiga mbili.

Takwimu hizo moja kwa moja zinaonyesha namna, Simba ilivyocheza chini zaidi ya wenyeji waliokuwa na mkakati wa kusaka mabao na kufanikiwa.

Katika mechi hiyo ambayo Simba inalazimika kuingia kwa mbinu za kushambulia zaidi ili kutafuta mabao ya mapema yatakayowarudisha kwenye morali ya juu, Fadlu hana budi kubadilisha aina ya wachezaji wa kuanza.

Ilionekana eneo la kiungo la Simba kuzidiwa nguvu katika mechi ya kwanza ambapo pale kati Fabrice Ngoma na Yusuph Kagoma, walishindwa kuwa imara mbele ya Mamadou Camara aliyefunga bao la kwanza na Ayoub Khairi. Uharaka wa viungo wa Berkane uliifanya timu hiyo kupanga mashambulizi kirahisi wakati Simba kwao ikiwa ngumu.

Simba inahitaji kiungo mwenye kasi na uwezo wa kupandisha mashambulizi kwa haraka, Debora Mavambo ambaye si mzuri sana katika kukaba, anaweza kutumika katika kupandisha mashambulizi kwani kazi hiyo anaiweza vizuri. Mavambo katika mchezo wa ugenini aliingia dakika za nyongeza baada ya tisini kukamilika akichukua nafasi ya Jean Charles Ahoua.

Lakini Elie Mpanzu aliwekwa chini ya ulinzi mkali, akakosa msaada hadi alipotolewa dakika ya 80 na kuingia Joshua Mutale, huku Kibu Denis naye akishindwa kuonyesha makali yake, mapema tu wakati kipindi cha pili kinaanza aliingia beki wa kushoto Valentine Nouma kuchukua nafasi yake. Nouma ni mzuri katika kupandisha mashambulizi, na pia anajua kukaba.

Mabadiliko hayo matatu, yalionyesha uhai kwa kiasi fulani ambapo ilishuhudiwa kipindi cha pili hakukuwa na bao baada ya yale mawili kufungwa ndani ya dakika 15 za kipindi cha kwanza.

Mutale ambaye ni winga, amekuwa akifanya vizuri katika mechi za hivi karibuni, hivyo anaweza kupewa nafasi akaonyesha kitu cha tofauti.

Mbali na eneo la kiungo kuhitaji mchezaji mwenye kasi na uwezo wa kupandisha timu, pale mbele Steven Mukwala ana nafasi kubwa ya kuanza katika uhitaji huo wa mabao ya mapema kwani mshambuliaji huyo licha ya kutokuwa na nguvu kama alizonazo Ateba, lakini ana uwezo wa kuwahamisha mabeki na kuwaachia mwanya viungo washambuliaji kuingia ndani na kumaliza kazi.

Mukwala alikuwa mshambuliaji muhimu akifunga bao moja wakati Simba ikipindua matokeo Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Al Masry katika mchezo wa robo fainali baada ya ugenini kufungwa 2-0, kisha nyumbani nao kushinda idadi hiyo ya mabao, ikaenda mikwaju ya penalti ambayo Simba ikashinda 4-1 na kufuzu nusu fainali.

Katika ulinzi, Simba imejitahidi kwani hadi sasa imeruhusu mabao tisa katika mechi 13, wachezaji wanaocheza eneo hilo kwa kiasi kikubwa ni walewale ambao ni kipa Moussa Camara, mabeki wa pembeni Shomari Kapombe na nahodha Mohamed Hussein, huku pale kati alikuwa akitumika Abdulrazack Hamza na Che Fondoh Malone kabla ya kuumia na kumpisha Chamou Karaboue, kupona kwa Che Malone, imemfanya Fadlu kuamua aanze na nani kati yao. Mchezo uliopita Hamza aliumia mapema dakika ya 23, Che Malone akaingia. Hata hivyo, Hamza na Kibu wamefanya mazoezi na wenzao kuonyesha wapo fiti kwa mechi hiyo ya Jumapili ambayo kombe litakuwa uwanjani.

Kulingana na hayo yote, nyota wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema kocha Fadlu alikuwa sahihi kumuanzisha Leonel Ateba katika mchezo wa kwanza eneo la ushambuliaji kutokana na uwezo wake wa kukaa na mpira mguuni, kushambulia na mikimbio iliyo sahihi, lakini marudiano anaweza kupanga kikosi kwa mfumo wa 4-4-2 ama kikacheza kilekile chenye mfumo wa 4-3-3.

“Mukwala ana kasi na mikimbio mizuri isipokuwa anashindwa kukaa na mali mguuni, tofauti na Ateba anaficha mpira mguuni, lakini sina shaka na kikosi kilichoanza ugenini kinaweza kikaanza na hapa pia, kocha ndiye anajua nani kaamka vizuri na kama mchezaji anaumwa aseme mapema,” alisema Batgol na kuongeza;

“Wachezaji wa Simba wajitolee kupambania nchi, wasicheze kama wapo kazini kuchukulia kirahisi, hiyo mechi ni ya kihistoria, naamini kuna uwezekano mkubwa wakapata mabao matatu kulingana na kile ambacho walikionyesha kipindi cha pili wakiwa ugenini.”

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Steven Mapunda ‘Garrincha’ alisema ili kupata matokeo mazuri kipindi cha kwanza, kocha Fadlu anapaswa kumuanzisha Joshua Mutale au Kibu, Elie Mpanzu na Mukwala, kisha Ateba aingie kipindi cha pili.

“Fadlu alikuwa sahihi kumchezesha Ateba, ugenini ndio maana alikuwa na uwezo wa kuondoka na watu kama watatu hadi wanne, hivyo wapinzani walikuwa wanaogopa kupanda juu, hao niliowataja Mutale, Kibu, Mpanzu na Mukwala wakianza kipindi cha kwanza katika mchezo huu wana uwezo wa kupata matokeo ya mabao mawili, ili kina Ateba wakiingia kipindi cha pili watafute bao la ushindi,” alisema Garrincha.

Kocha Julien Chevalier anayeifundisha ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambaye timu yake iling’olewa na Berkane katika robo fainali ya michuano hiyo kikifungwa jumla ya mabao 2-0, ikichapika ugenini 1-0 na nyumbani pia, alisema Fadlu anatakiwa kuimarisha ulinzi na kuuanza mchezo huo kwa kasi akiwapa nafasi wachezaji wanaoweza kushambulia kwa haraka.

Kheireddine Madoui wa CS Constantine ya Algeria ambaye ndiye kocha pekee aliyeifunga Berkane kwenye michuano hiyo msimu huu hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa 1-0 nyumbani baada ya ugenini kulala 4-0, alisema Simba haitakiwi kurudia makosa ya safu yao ya ulinzi. Wanatakiwa kuwa imara kwenye ulinzi lakini pia wasisubiri Berkane iamue kasi ya mchezo, wanatakiwa kuanza, yule mshambuliaji wa Uganda (Mukwala) ana kasi.”

“Nadhani anatakiwa kuanza lakini pia ana nguvu, Simba inatakiwa kuicheza kwa nguvu mechi hiyo kwa asilimia mia moja, hii itawaweka kwenye wakati mgumu Berkane.”

Kheireddine Madoui alisema anafahamu Berkane itaingia na akili ya kucheza soka la kushambulia kwa kushtukiza na haitakuwa nzuri kwa Simba kuruhusu bao kwenye mchezo huo.

“Tulipocheza nao Berkane, tulifanya makosa kwenye ulinzi tukaruhusu mabao mengi mchezo wa kwanza ugenini, lakini Simba haikufanya makosa mengi, hayo mabao mawili wanaweza kuyarudisha.

“Sijajua yule aliyetufunga bao la pili kwenye mchezo wa marudiano hatua ya makundi (Kibu Denis) sijui kwanini amepungua kasi.

“Kama kocha wao (Fadlu) atazungumza naye na akacheza kwa kuchangamka wanaweza kuweka presha nzuri kwa Berkane, wanatakiwa kucheza kwa akili na ujasiri mkubwa, tuliwafunga Berkane hapa lakini haikutosha kwani tulishafanya makosa makubwa kupoteza vibaya kule kwao.”