Mwamba Modrid anasepa Real Madrid

Muktasari:
- Modric ambaye alijiunga na Madrid akitokea Tottenham Hotspur, kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyeshinda mataji mengi zaidi katika historia ya timu hiyo.
MADRID, HISPANIA: STAA wa Real Madrid, Luka Modric, mwenye umri wa miaka 39, ametangaza kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia kwa miaka 13.
Modric ambaye alijiunga na Madrid akitokea Tottenham Hotspur, kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyeshinda mataji mengi zaidi katika historia ya timu hiyo.
Kwa jumla, Modric ambaye pia aliwahi kutwaa tuzo ya Ballon d'Or mwaka 2018, ameshinda mataji 28 akiwa na Real Madrid.

Staa huyo amewaaga mashabiki wa timu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo ameandika: "Mashabiki wapendwa wa Real Madrid wakati wangu umefika. Wakati ambao sikuwa nataka ufike, lakini huo ndio mpira, na katika maisha kila kitu kina mwanzo na mwisho. Jumamosi nitacheza mechi yangu ya mwisho kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu."
"Nilifika mwaka 2012 nikiwa na shauku ya kuvaa jezi ya timu bora duniani na kwa matarajio ya kufanya mambo makubwa, lakini sikuweza kufikiria kilichofuata."

"Kucheza Real Madrid kulibadilisha maisha yangu kama mchezaji wa soka na kama mtu binafsi. Najivunia kuwa sehemu ya mafanikio makubwa zaidi ya klabu hii bora katika historia. Ninataka kumshukuru kutoka moyoni mwangu, rais Florentino Perez, wachezaji wenzangu, makocha na watu wote waliokuwa nami na kunisaidia katika kipindi chote hiki."
Akiwa Real Madrid, kiungo huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur ameshinda mataji manne ya LaLiga, sita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mawili ya Copa del Rey pamoja na mengine ya michuano mbalimbali.

Mwezi uliopita, Modric alifichua kuwa angependa kustaafu akiwa Real Madrid, aliposema: "Ndiyo, ningependa kustaafu Real Madrid, itakuwa ndoto iliyotimia kwangu."
Hivi karibuni, Modric pia alitangazwa kuwa mmoja wa wamiliki wapya wa Swansea City inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza England.