Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Scaloni aingiwa hofu kuhusu Messi Kombe la Dunia 2026

Muktasari:

  • Messi mwenye umri wa miaka 38 ameitwa kwenye kikosi cha Argentina kwa ajili ya mechi za kirafiki katika kipindi hiki cha kalenda ya Fifa ambapo jana walitarajiwa kukipiga dhidi ya Mauritania kisha Zambia, Jumatano ijayo, Aprili Mosi, ambapo wakati akiripoti timu ya taifa aliibua vaibu kwa mashabiki wa Argentina.

BUENOS AIRES, ARGENTINA: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni, ni kama ameingiwa na hofu kufuatia kauli yake kwamba hana uhakika wa nahodha wake, Lionel Messi, kama atacheza fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026 ikiwa imebaki takriban miezi miwili.

Messi mwenye umri wa miaka 38 ameitwa kwenye kikosi cha Argentina kwa ajili ya mechi za kirafiki katika kipindi hiki cha kalenda ya Fifa ambapo jana walitarajiwa kukipiga dhidi ya Mauritania kisha Zambia, Jumatano ijayo, Aprili Mosi, ambapo wakati akiripoti timu ya taifa aliibua vaibu kwa mashabiki wa Argentina.

Scaloni ameweka wazi kwamba Messi atashiriki mechi hizo za kirafiki, lakini bado kuna shaka kama atakuwa sehemu ya kikosi cha Argentina katika mpango wa kutetea ubingwa wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia, ambayo itaanza Juni 17, ikichezwa Marekani, Canada na Mexico, ambapo mechi ya kwanza kwa wababe hao kutoka America Kusini itakuwa dhidi ya Algeria huko Kansas City.

“Hili ni swali gumu kwangu; nadhani linamhusu zaidi yeye (Messi), lakini kwa upande wangu nadhani mnajua nini nahitaji. Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha tunakuwa naye kikosini,” alisema Scaloni.

“Naamini lazima awepo, kwa ajili ya mpira wa miguu, lakini mwisho wa siku sio mimi nacheza nafasi ya kuamua. Yeye ndiye anaamua, jinsi anavyohisi. Ni vigumu kwa sababu sio Wargentina pekee wanataka kumuona; kila mtu anataka kumuona. Kisha sisi kama makocha tunatazama kama atakapokuwepo, kama atakuwa na nguvu ya kucheza mchezo mzima au la.”

Scaloni aliongeza: “Sitaweka masharti hapa kusema kwamba lazima nitamchague au la kwenye kikosi changu. Amefanya kazi ngumu na ana haki ya kuamua kwa utulivu. Hatuna haraka. Tunajua uamuzi wake utakuwa bora kwake na timu. Tunaimani atakuwa nasi, lakini siwezi kusema zaidi.”

Hadi sasa Messi ameshiriki katika mashindano matano ya Kombe la Dunia (2006, 2010, 2014, 2018 na 2022) na amekuwa mchezaji aliyeonekana mara nyingi zaidi katika fainali za Kombe la Dunia kwa mchezaji yeyote (mechi 26).

Pia amefunga mabao 13 katika Kombe la Dunia, idadi ambayo ni ya juu kabisa kwa Argentina.

Oktoba iliyopita, Messi, ambaye kwa sasa anaichezea Inter Miami, alikiri kuwa hana hakika kama atakuwa sehemu ya kikosi cha Argentina katika fainali hizo, ambazo kwa mara ya kwanza zinaandaliwa kwa ushirikiano wa mataifa matatu tofauti.

“Ni jambo gumu kusema kwamba nitakuwa sehemu ya Kombe la Dunia, na ningependa kuwa hapo, lakini itategemea na hali yangu kiafya,” alisema Messi.

Messi ndiye mfungaji bora wa historia ya timu ya taifa ya Argentina akiwa na mabao 115 katika mechi za kimataifa tangu 2005 (zikiwamo za kirafiki, akicheza mechi 197 ikiwa ni rekodi ya juu kwa taifa hilo.

Kwa klabu ya sasa, Inter Miami, Messi pia amefanya makubwa tangu kujiunga nayo akitokea PSG ya Ufaransa, amekuwa mfungaji bora wa klabu (mabao 82) katika historia yake na anakuwa mchezaji mwenye asisti nyingi zaidi (53) kwa rekodi ya klabu, akisaidia timu kushinda mataji makubwa ikiwa ni pamoja na Leagues Cup, Supporters’ Shield na MLS Cup.

Zaidi ya hayo, Messi amekuwa mchezaji wa pili wa kiume kufikia mabao 900 kwa klabu na timu ya taifa.