Sane bado anaiwaza EPL

Muktasari:
- Sane ambaye mkataba wake na Bayern unamalizika mwisho wa msimu huu, alicheza England akiwa na Manchester City chini ya Pep Guardiola kwa misimu mitatu akishinda mataji mbalimbali yakiwemo matatu ya Ligi Kuu nchini humo.
MUNICH, UJERUMANI: STAA wa Bayern Munich, Leroy Sane amesema bado anatazama na anaipenda Ligi Kuu England hali inayozidisha tetesi kwamba anaweza kutua Arsenal au Manchester United zinazohusishwa kutaka kumsajili.
Sane ambaye mkataba wake na Bayern unamalizika mwisho wa msimu huu, alicheza England akiwa na Manchester City chini ya Pep Guardiola kwa misimu mitatu akishinda mataji mbalimbali yakiwemo matatu ya Ligi Kuu nchini humo.
Staa huyu amesema ni kweli anaipenda ligi ya EPL na bado anatazama baadhi ya mechi lakini kwa sasa hana mpango wa kurejea kwenye ligi hiyo kwani bado ana mkataba na Bayern.
Mbali ya Arsenal na Manchester United, fundi huyu pia amewahi kuhusishwa na Newcastle ambazo zote zina matumaini ya kumpata mwisho wa msimu.
“Nina upendo na ligi hiyo, bado natazama michezo fulani kwenye televisheni. Lakini akili yangu ipo kwenye klabu ambayo naweza kuonyesha ubora wangu, kukua kimchezo na kushinda mataji ambayo ni Bayern. Hapa kwa sasa ndiko ninakopata nafasi ya kucheza kwa ajili ya kutimiza malengo yangu,” alisema Sane alipofanya mahojiano na tovuti ya SportBild.
Sane anaweza kuonekana tena uwanjani akiitumikia Bayern kesho usiku watakapokutana na Augsburg katika mchezo wa Bundesliga.
Mara kadhaa ripoti zimeeleza kuwa Bayern inafanya mchakato wa kuingia katika mazungumzo na wawakilishi wake ili kumsainisha mkataba mpya lakini hadi sasa hakuna maendeleo yoyote juu ya hilo.
Timu za Hispania hususani Barcelona nayo imetajwa kutaka kumsajili staa huyu wa kimataifa wa Ujerumani.