Prime
Kigogo TFF atia neno fainali CAFCC kuchezwa Zanzibar

Muktasari:
- Kila shabiki wa Simba na mzalendo anatamani kusikia Wekundu hao hao wanapewa ruhusa ya kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mchezo wa marudiano, lakini taarifa za uhakika, hilo halitaweza kutimia. Taarifa za uhakika kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni, CAF haina hata nafasi ya kubadili maamuzi ya kubadili uwanja wa mchezo huo.
SIMBA imerejea nchini ikitokea Morocco ilikopoteza mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya RS Berkane kwa mabao 2-0.
Mabao ya dakika 15 za kwanza ya Berkane kwenye Uwanja wa Manispaa ya mji wa Berkane, yaliiweka timu hiyo katika nafasi nzuri ya kubeba taji kwa mara ya tatu, lakini Fadlu ametamba mechi ijayo itakuwa tofauti, huku rekodi ya Simba nyumbani ikiibeba dhidi ya Berkane ugenini ikimpa matumaini.
Kila shabiki wa Simba na mzalendo anatamani kusikia Wekundu hao hao wanapewa ruhusa ya kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mchezo wa marudiano, lakini taarifa za uhakika, hilo halitaweza kutimia. Taarifa za uhakika kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni, CAF haina hata nafasi ya kubadili maamuzi ya kubadili uwanja wa mchezo huo.
Kigogo mmoja wa juu kutoka TFF (jina tunalo) aliliambia Mwanaspoti CAF haitaweza kubadili uamuzi uliopo sasa kutokana na kabla ya kuamua fainali hiyo kupigwa Uwanja wa New Amaan, vilifanyika vikao vya wiki mbili juu ya maamuzi hayo.
Kigogo huyo aliongeza mara baada ya CAF kumaliza kufanya maamuzi hayo wahusika wote walijulishwa na sasa Maofisa wa Idara ya mashindano kutoka CAF tayari wanaendelea na maandalizi hayo.
“Hakutawezekana kubadilika kitu, hata sisi tunatamani hilo litokee, lakini ile ni CAF wakiamua huwa wanasimamia kile walichoamua, mchezo utapigwa Uwanja wa Amaan Zanzibar,” alisema bosi huyo na kuongeza;
“Mnatakiwa kuwasaidia Simba, waache kujiondoa mchezoni, wajipange kucheza New Amaan, bado wanaweza kufanya vizuri, kuendelea kuonyesha hawatashinda kule Zanzibar ni kuwaharibu kisaikolojia wachezaji wao.
“Vilifanyika vikao vingi kabla ya maamuzi haya lakini kwasasa kwa kuwa maamuzi yameshafanyika na ripoti zimeshakwenda kwao (CAF) hakutaweza kuwa na mabadiliko, hata wao wenyewe (CAF) wameshatoa taarifa mchezo utapigwa New Amaan.”
Simba itakabiliana na Berkane ikiwa na deni la kurudisha mabao 2-0, iliyofungwa juzi kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, ikisaka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kubeba taji la Afrika baada ya awali kushindwa kulibeba Kombe la CAF mwaka 1993 na Yanga kukwama kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 mbele ya USM Alger ya Algeria kwa kanuni ya bao la ugenini.