Samatta ndo kaanza na neema Ubelgiji

NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameanza na neema huko Ubelgiji baada ya chama lake jipya Royal Antwerp kuibuka na ushindi kwenye mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge nalo kwa mkopo wa msimu mzima akitokea Fenerbahce SK.

Samatta ambaye siku chache zilizopita aliisaidia Taifa Stars kuibuka na ushindi wake wa kwanza dhidi ya Madagascar kwenye harakati za kupigania nafasi ya kwenda Qatar mwakani kucheza kombe la Dunia, alipewa nafasi kwenye mchezo huo.

Licha ya ugeni wake kwenye klabu hiyo, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania akiwa amevalia jezi namba 70, alionekana akipasha mwanzoni mwa kipindi cha pili huku mashabiki wakimpigia makofi kama ishara ya kumkubali.

Samatta anakumbukwa vizuri na mashabiki wa soka Ubelgiji kutokana na kile ambacho alikifanya msimu wa 2018/19 ambapo aliisaidia KRC Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Jupiler Pro.

Shangwe la mashabiki hao lilizidi dakika ya 56 baada ya kuonekana mshambuliaji huyo wa Kitanzania akiingia kuchukua nafasi ya Benson Hedilazio wakati huo, Royal Antwerp walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Mswiss, Michael Frey.

Kwa dakika 34 ambazo amecheza Samatta alionekana kufanya vizuri licha ya ugeni wake na anaonekana anaweza kufanya vizuri zaidi kadri ambavyo atakuwa akizoeana na wachezaji wenzake. Royal Antwerp inatiketi ya kucheza Europa Ligi.

Katika michuano ya Europa Ligi, Royal Antwerp wapo kundi moja D na klabu iliyomtoa Samatta kwa mkopo, Fenerbahce SK sambamba na vigogo wengine kwenye soka nla Ulaya ambao ni Frankfurt ya Ujerumani na Olympiacos ya Ugiriki.