Safari imeiva, Bruno aletewa mtu
Muktasari:
- Sasa kinachoelezwa ni mabosi wa Manchester United wanafikiria kwenda kumnasa kiungo wa Juventus, Kenan Yildiz ili kuja kuziba pengo litakaloachwa na Mreno huyo.
MANCHESTER, ENGLAND: NDO hivyo. Lisemwalo ni miamba ya soka ya Saudi Arabia, ambayo ni Al-Hilal, Al-Nassr na Al-Ittihad imedhamiria kutua Old Trafford dirisha lijalo la majira ya kiangazi kumnasa Bruno Fernandes.
Sasa kinachoelezwa ni mabosi wa Manchester United wanafikiria kwenda kumnasa kiungo wa Juventus, Kenan Yildiz ili kuja kuziba pengo litakaloachwa na Mreno huyo.
Huko kwenye kikosi cha Man United wameanza kuwa na wasiwasi huenda kiungo huyo mchezeshaji akashawishika na mpango wa kuondoka Old Trafford wakati wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwishoni mwa msimu huu.
Wachezaji hao wa Man United wanaamini nahodha wao amechoshwa na mapito yote kwenye klabu hiyo, hivyo atatafuta mwanzo na changamoto mpya katika kuelekea kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika majira ya kiangazi yajayo huko Marekani, Canada na Mexico.
Kiungo huyo wa Kireno, Bruno mwenye umri wa miaka 31 alifichua Novemba mwaka jana Kocha Ruben Amorim alimshawishi abaki kwenye kikosi hicho wakati wa dirisha lililopita la majira ya kiangazi wakati miamba ya Saudi Arabia, Al-Hilal ilipoweka mezani ofa ya Pauni 100 milioni.
Amesema alihisi kuumia na kuhuzunika sana kwa sababu mabosi wa Man United walidhamiria kumpiga bei kwenye dirisha hilo.
Fernandes amesema: “Kitu nilichokihisi ilikuwa hivi, ‘kama utaondoka haitakuwa mbaya kwetu’.
“Hilo liliniumiza sana. Nadhani hawakuwa na ujasiri wa kufanya uamuzi kama ambao kocha amefanya kwa ajili yangu.”
Baada ya hapo, kiungo Fernandes alidai hatafikiria juu ya hatima ya soka lake hadi hapo fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakapomalizika.
Lakini, baadhi ya wachezaji wenzake wanadhani kiungo huyo tayari akilini ana jambo lake.
Chanzo kilichofichua hilo kilibainisha: “Baadhi ya wachezaji kwenye kikosi wanadhani Bruno ameshachoka, kwa kusema ukweli, hawamlaumu. Amejitolea kwa zaidi ya asilimia 100 na amekuwa mchezaji bora wa timu tangu alipojiunga.
“Lakini, anahisi kuangushwa na uongozi mpya na ishu ya kuondoka Amorim ndiyo kabisa imetibua. Hakuna kabisa mtu wa kushawishika na pesa nyingi kuhamia Saudia, yeye ni mtu wa soka halisi. Hakuna mtu atamtilia shaka kutoka siku aliyosaini Man United, amejitolea kwa kila kitu.
“Hakuna anayemtaka aondoke, lakini wachezaji wenzake watamwelewa endapo kama atafanya hivyo.”
Fernandes alijiunga na Man United, dirisha la Januari 2020 kwa ada ya Pauni 46.6 milioni akitokea Sporting Lisbon na mkataba wake huko Old Trafford utafika tamati 2027.
Akirejea kutoka kwenye majeraha, Fernandes alicheza mechi ya sare ya mabao 2-2 kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Burnley, wakati kikosi hicho kikiwa chini ya kocha wa mpito Darren Fletcher na alianzishwa pia katika mechi ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Brighton kwenye Kombe la FA na kusukumwa nje ya michuano hiyo.
Rekodi za Fernandes kwenye Ligi Kuu England, amecheza mechi 213, huku ni mara nne tu ndiyo alizotokea benchini, amefunga mabao 67 na kuasisti 59.
Amegusa mpira ndani boksi la timu pinzani mara 661, amepiga penalti 30 na kufunga 24, amegongesha mwamba mara 25, amecheza rafu 210 na kuonyeshwa kadi za njano 38 huku mara mbili tu ndizo alizotolewa uwanjani kwa kadi nyekundu.