Bruno Fernandes awatia hofu mastaa Man United
Muktasari:
- Wachezaji wa klabu hiyo, wanaamini Bruno amechoshwa na maendeleo ya klabu na atatafuta timu nyingine baada ya Kombe la Dunia 2026.
MANCHESTER, ENGLAND: MASTAA wa Manchester United wameingiwa hofu kwa nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes kuchoshwa na mambo yanayoendelea kikosini na huenda anaweza kutaka kuondoka kupitia dirisha lijalo la majira haya ya kiangazi.
Wachezaji wa klabu hiyo, wanaamini Bruno amechoshwa na maendeleo ya klabu na atatafuta timu nyingine baada ya Kombe la Dunia 2026.
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 31, alikiri Novemba mwaka jana kuwa kocha wa wakati huo, Ruben Amorim, alimshawishi abaki katika dirisha la majira ya kiangazi lililopita wakati klabu ya Saudi Arabia, Al-Hilal, ilipowasilisha ofa ya Pauni 100 milioni ili kumsajili.
Pia alifichua jinsi alivyoumia na kusikitika kwa sababu alihisi kuwa viongozi wa Man United walikuwa tayari kumuuza na kupokea ofa hiyo.
Kiungo huyo alisema: "Kwa upande wa klabu nilihisi ilikuwa kama, ‘Ukiondoka si tatizo kubwa kwetu.’
“Hilo linaniumiza kidogo… nahisi hawakuwa na ujasiri wa kufanya uamuzi tofauti na ule wa kocha ambaye alitaka nibaki."
Tangu wakati huo, Fernandes amesisitiza hatofikiria kuhusu mustakabali wake hadi baada ya kucheza Kombe la Dunia litakalofanyika mwaka huu huko Marekani, Mexico na Canada.
Hata hivyo, baadhi ya wachezaji wenzake wanaamini kuwa nyota huyo tayari ameshafanya uamuzi wake.
Chanzo kimoja kilisema: "Baadhi ya wachezaji kikosini wanaamini Bruno amechoka, na kwa kweli hawamlaumu. Daima hujitoa kwa asilimia 100 na amekuwa mchezaji bora wa klabu tangu alipojiunga.
"Lakini wanaamini anahisi kudharauliwa chini ya mfumo mpya wa umiliki wa klabu. Yeye si mchezaji anayevutiwa sana na dili la pesa nyingi la kwenda Saudi kwa sababu yeye ni mpenda soka na anataka kucheza ligi kubwa siku zote."
Fernandes alijiunga na Man United mwaka 2020 kwa ada ya Pauni 46.6 milioni kutoka Sporting Lisbon ya nchini kwao Ureno, na mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027.
Alirejea kikosini kwenye sare ya mabao 2-2 ya Ligi Kuu dhidi ya Burnley Jumatano na alikuwapo pia katika kikosi cha kocha wa mpito Darren Fletcher kilichocheza dhidi ya Brighton katika Kombe la FA leo.
Hadi sasa viongozi wa Man United bado hawajafikia uamuzi kuhusu nani atakuwa kocha wa mpito kwa kipindi cha msimu kilichosalia ingawa kuna uwezekano mkubwa wakamteua Ole Gunnar Solskjaer au Michael Carrick.
Kwa sasa kikosi hicho kipo chini ya Fletcher ambaye kabla ya hapo alikuwa kocha wa kikosi cha vijana wa chini ya miaka 18 kuanzia mwaka jana.
Staa huyu wa zamani wa Man United kwa mara ya kwanza alirejea Man United Januari 2021 kama kocha kabla ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi wao wa kwanza wa ufundi miezi miwili baadaye.
Alipoulizwa kama alishangazwa kutoteuliwa kuwa kocha wa mpito kwa msimu mzima, Fletcher (41) alisema:
“Hapana, nilishangazwa kuteuliwa kwa michezo miwili kwa sababu sikutarajia kabisa. Mimi sifikirii kwanini hawajanichagua niongoze msimu mzima, mimi naangalia kilicho mbele yangu. Kwanza kuteuliwa tu kulinishangaza kwa sababu haikuwa kabisa kwenye mipango yangu. Lakini ninapoulizwa kuifanya kazi hii nilisema naweza. Ninaifahamu mazingira yaliyopo hapa na naamini uwezo wangu. Nahisi nimejifunza mengi katika miaka mitano niliyokuwapo hapa.
“Nimepata uzoefu mzuri kama mchezaji. Nimechukua muda wangu kujiendeleza na kujifunza kama kocha na pia mambo mengine nje ya uwanja.
“Nafurahi nimefanya hivyo, kwa sababu imenipa nafasi nzuri sasa au nafasi bora zaidi kuliko ile niliyokuwa nayo miaka mitano iliyopita."