Rooney: Arteta? Kibarua kigumu
Muktasari:
- Arsenal sasa ni vinara wa kubashiriwa kushinda taji lao la kwanza la ligi tangu mwaka 2004. Na kwa kuwa Arsenal ipo katika nafasi nzuri kabisa, Rooney anaona hakuna kisingizio iwapo kikosi cha Arteta kitashindwa kukamilisha kazi.
LONDON, ENGLAND: GWIJI wa Ligi Kuu England, Wayne Rooney anaamini Mikel Arteta anaweza kufukuzwa kazi iwapo hatafanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu England msimu huu.
Kikosi cha Arteta kinaongoza msimamo wa ligi kwa pointi sita mbele ya Manchester City.
Arsenal sasa ni vinara wa kubashiriwa kushinda taji lao la kwanza la ligi tangu mwaka 2004. Na kwa kuwa Arsenal ipo katika nafasi nzuri kabisa, Rooney anaona hakuna kisingizio iwapo kikosi cha Arteta kitashindwa kukamilisha kazi.
Staa huyo wa zamani wa England na Manchester United, alikiambia kipindi cha ‘The Wayne Rooney Show’: “Nadhani hata kwa Arteta pia, kama hawatashinda mwaka huu, basi unajua Arsenal wamemuunga mkono kwa kiasi kikubwa sana, hasa msimu huu na wamempa kikosi kizuri sana. Kwa hiyo kama hawatashinda mwaka huu, nadhani kutakuwa na presha kubwa kwa Arteta hakika kabisa.”
Rooney pia anaamini kuwa ushindi wa kusisimua wa Manchester City dhidi ya Liverpool huko Anfield, Jumapili unaweza kuwa umevuruga mawazo ya Arteta.
Liverpool ilikuwa mbele kwa bao moja zikiwa zimesalia dakika 16, lakini waliruhusu Man City kurejea mwishoni mwa mchezo na kushinda 2-1. Kama Man City ingeshindwa wikiendi iliyopita, ingeachwa nyuma na Arsenal kwa pointi tisa.
Rooney aliongeza: “Athari yake inaweza kuwa kubwa sana, kwa sababu nakumbuka tulipokuwa (Manchester United) kwenye mbio za ubingwa, ukicheza Jumamosi au mapema na kushinda, halafu unaona pengo linapungua kutoka pointi tisa hadi sita. Na namna ilivyotokea pia kwa sababu Liverpool inaongoza kwa bao, unafikiri kama hali itabaki hivyo na pengo liwe pointi tisa, hiyo ni motisha kubwa kwetu.”