Ronaldo kupewa miwili huko

Muktasari:
- Inaeleweka kuwa mazungumzo yanaendelea kuhusu mkataba mpya ambao utamwezesha mshindi huyo wa mara tano wa Ballon d’Or kuendelea kucheza hadi atakapokuwa na umri wa miaka 42.
RIYADH, SAUDI ARABIA: STAA wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo anatarajiwa kusaini mkataba mpya na Al Nassr ya Saudi Arabia ambao utamwezesha kusalia kwenye timu hiyo hadi mwaka 2027, licha ya tetesi zilizodai kwamba anaweza kuondoka.
Inaeleweka kuwa mazungumzo yanaendelea kuhusu mkataba mpya ambao utamwezesha mshindi huyo wa mara tano wa Ballon d’Or kuendelea kucheza hadi atakapokuwa na umri wa miaka 42.
Ronaldo alijiunga na Al Nassr Januari 2023 baada ya kuondoka Manchester United kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wake.
Licha ya kulipwa mshahara mkubwa unaozidi pauni 100 milioni kwa mwaka, Ronaldo bado hajafanikiwa kuipa timu hiyo taji.
Hivi karibuni alifunga bao katika mechi ya mwisho ya msimu ambapo Al Nassr ilipoteza 3-2 dhidi ya Al-Fateh, na kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Baada ya mechi hiyo, shughuli zake za mitandaoni ziliibua maswali aliposema: “Kipindi hiki kimeisha. Hadithi? Bado inaandikwa. Ninamshukuru kila mtu.”
Wengi walitafsiri maneno hayo kama ishara ya kuaga Al Nassr, timu ambayo haijapata mafanikio makubwa ya vikombe tangu kuwasili kwake.
Hata hivyo, inaonekana sasa atabaki, licha ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kusema awali kuwa Ronaldo huenda angejiunga na klabu nyingine ili kushiriki Kombe la Dunia la Klabu.
Ronaldo amefunga mabao 99 katika mechi 111 akiwa na Al Nassr, lakini mafanikio hayo binafsi hayakuisaidia timu yake.
Tangu aondoke Juventus miaka mitano iliyopita, Ronaldo hajawahi kucheza katika kikosi kilichotwaa ubingwa wa ligi.
Umri wake mkubwa na mahitaji makubwa ya kifedha vimekuwa kikwazo kwa timu nyingi zinazohitaji kumsajili.