Ronaldo amfariji mtoto aliyenusurika tetemeko, amwalika kumtazama akicheza
Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, alimtumia kijana huyo, Andres, maneno ya kumtia moyo kabla ya kumwalika kukutana naye ana kwa ana.
MIAMI, MAREKANI; CRISTIANO Ronaldo amemtumia ujumbe wa kumfariji moyo mvulana wa Venezuela aliyepoteza kila kitu kutokana na tetemeko la ardhi la hivi karibuni.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, alimtumia kijana huyo, Andres, maneno ya kumtia moyo kabla ya kumwalika kukutana naye ana kwa ana.
Baada ya kuona ujumbe wa mvulana huyo aliyepoteza kila kitu kufuatia tetemeko la ardhi, Ronaldo alichukua hatua mara moja.
Mbali na kumtia moyo kwa maneno ya faraja, alimwalika Andres kuhudhuria moja ya mechi zake akisema”nataka uje kutazama moja ya mechi zangu!”
Inaaminika kuwa Ronaldo aliona ujumbe wa mtoto huyo na kuamua kuwasiliana naye binafsi.
Video iliyosambaa inaonyesha kijana huyo akionyeshwa ujumbe wa Ronaldo, huku uso wake ukijaa tabasamu la furaha na matumaini.
Hadi sasa haijafahamika kama familia ya mvulana huyo ilinusurika katika janga hilo la asili.
Mnamo Juni 24, Venezuela ilikumbwa na matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyosababisha uharibifu mkubwa.
Matetemeko hayo, yaliyokuwa na ukubwa wa 7.2 na 7.5 katika kipimo cha Richter, yalitikisa maeneo ya pwani na kusababisha majengo mengi kuporomoka.
Yalitokea kwa tofauti ya sekunde 39 tu na katika kina cha chini ya kilomita 25 kutoka usawa wa ardhi, huku tetemeko la ukubwa wa 7.5 likiwa ndilo kubwa zaidi kuikumba Venezuela katika zaidi ya miaka 100.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizotolewa Ijumaa, idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na matetemeko hayo imefikia 2,645, huku zaidi ya 12,600 wakijeruhiwa.
Ujumbe wa Ronaldo kwa shabiki huyo mdogo umefika muda mfupi baada ya kuiongoza timu yake kuiondoa Croatia kwenye mashindano na kufuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41 alifunga bao lake la 146 akiwa na timu ya taifa katika ushindi wa mabao 2-1, na kufikisha jumla ya mabao 976 katika maisha yake yote ya soka.
Sasa anatarajiwa kuiongoza timu yake katika mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Hispania.
Hata hivyo, bado haijulikani kama Andres ataweza kuhudhuria Kombe la Dunia, kwani anaendelea kupata matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa katika tetemeko hilo.
Iwapo hatafanikiwa kwenda Kombe la Dunia, huenda siku moja akasafiri hadi Saudi Arabia kumshuhudia Ronaldo akicheza akiwa na klabu ya Al-Nassr.