Robert Lewandowski, Juventus wana jambo lao
Muktasari:
- Taarifa zinadai Juventus inataka kumsajili fundi huyo kwa usajili huru mwisho wa msimu pale mkataba wake wa sasa utakapokuwa unamalizika.
INAELEZWA Juventus imeanza kufanya jitihada za kumsajili mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Poland, Robert Lewandowski mwenye umri wa miaka 37kuelekea dirisha lijalo la majira kiangazi.
Taarifa zinadai Juventus inataka kumsajili fundi huyo kwa usajili huru mwisho wa msimu pale mkataba wake wa sasa utakapokuwa unamalizika.
Hadi sasa bado hakuna taarifa rasmi juu ya hatma yake katika kikosi cha Barca ingawa inaaminika mazungumzo yanaendelea.
Inaelezwa kwamba awali Barca ilikuwa inataka kuachana na Lewandowski ili kupata nafasi ya kumsainisha mkataba wa moja kwa moja Marcus Rashford, lakini baada ya kuona mambo yamekuwa magumu imesitisha mpango wa kumruhusu nyota huyo kuondoka.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Lewandowski amecheza mechi 37 za michuano yote, amefunga mabao 16 na kutoa asisti mara tatu.
Mabosi wa Juventus wapo tayari kumpa mshahara wa hadi Pauni 200,000 kwa wiki ili akubali kujiunga mwisho wa msimu.
Carlos Baleba
BRIGHTON huenda ikakubali kulegeza kamba kuhusu kiungo wa kimataifa wa Cameroon, Carlos Baleba, 22. Awali, Brighton ilikuwa ikitaka ada ya Pauni 100 milioni ili kumuuza staa huyo, lakini sasa ipo tayari kusikiliza ofa ambazo zitakuwa chini ya kiasi hicho cha pesa. Hatua hiyo inatajwa kuwa huenda ikaufungua mlango kwa klabu mbalimbali kuingia kwenye mbio za kumsajili Baleba ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2028.
Adam Wharton
KIUNGO wa kimataifa wa England, Adam Wharton, 22, anatajwa kuwa na mpango wa kuondoka Crystal Palace mwishoni mwa msimu huu.Inaelezwa kuwa Manchester United ambayo ni miongoni mwa timu zinazomuwania ina asilimia kubwa ya kumsajili kwani moja kati ya masharti aliyoipa ni kuhakikisha inafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya jambo ambalo linaonekana kuwapo kwa zaidi ya asilimia 70 kutokana nafasi katika ligi. Wharton ni miongoni mwa viungo bora Ulaya.
Aurelien Tchouameni
MANCHESTER United na Liverpool zinamfuatilia kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, Aurelien Tchouameni, 26, anayekipiga Real Madrid. Inaelezwa zote mbili zinataka kuimarisha safu za kiungo, na Tchouaméni anaonekana kuwa chaguo bora kutokana na uwezo wake. Hata hivyo, Real Madrid haionekani kuwa na mpango wa kumuuza licha ya kutopata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Elliot Anderson
ARSENAL inaendelea kuangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Nottingham Forest, Elliot Anderson, 23, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Hata hivyo, Arsenal haitakuwa peke yake katika mbio hizo, kwani Manchester City, Manchester United na Chelsea ni miongoni mwa timu zinazotajwa kutaka kumsajili. Anderson ameonyesha kiwango bora akiwa na Forest msimu huu licha ya timu yake kutokuwa na mwenendo mzuri.
Greenwood
JUVENTUS imeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Marseille, Mason Greenwood, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Hata hivyo, inatarajiwa kukutana na upinzani kutoka Atletico Madrid ambayo inaonekana kuwa mbele katika mbio na imeshazungumza hadi na wawakilishi wa mchezaji. Hatma ya Greenwood katika kikosi cha Marseille haijajulikana ingawa inaaminika kwamba mwenyewe anatamani kuondoka.
Ferran Torres
MANCHESTER United imepewa nafasi ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania, Ferran Torres, 26, kutoka Barcelona dirisha lijalo la kiangazi. Inaelezwa Barca iko tayari kusikiliza ofa jambo linaloweza kuipa Man United nafasi ya kumsajili na kuimarisha safu ya ushambuliaji. Torres aliyewahi kucheza Man City, kwa sasa hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha Barca.
Khvicha Kvaratskhelia
LIVERPOOL na Arsenal zimekumbana na pigo baada ya juhudi za kumsajili winga wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Georgia, Khvicha Kvaratskhelia, 25, kukwama. Inaelezwa kuwa PSG haina mpango wa kumuachia nyota huyo ambaye anaendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi chake kutokana na kiwango chake. Hatua hiyo inazilazimisha klabu hizo mbili kutafuta mbadala mwingine katika soko la usajili.