Rice apiga mbili, Arsenal ikijikita kileleni
Muktasari:
- Beki imara wa Arsenal, Gabriel alifanya makosa kuwapa Bournemouth bao la mapema dakika ya 10 baada ya kupiga pasi ya kipofu katikati iliyomkuta Evanilson, ambaye aliweka mpira nyavuni kwa utulivu. Lilikuwa ni kosa kubwa lisilo la kawaida kwa Mbrazili huyo, lakini alijirekebisha dakika tano na sekunde 18 baadaye alipoifungia Arsenal bao la kusawazisha.
LONDON, ENGLAND: DECLAN Rice alifunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza baada ya kupona jeraha, akiiongoza Arsenal kupata ushindi muhimu ugenini dhidi ya Bournemouth wakishinda 3-2.
Beki imara wa Arsenal, Gabriel alifanya makosa kuwapa Bournemouth bao la mapema dakika ya 10 baada ya kupiga pasi ya kipofu katikati iliyomkuta Evanilson, ambaye aliweka mpira nyavuni kwa utulivu. Lilikuwa ni kosa kubwa lisilo la kawaida kwa Mbrazili huyo, lakini alijirekebisha dakika tano na sekunde 18 baadaye alipoifungia Arsenal bao la kusawazisha.
Rice alifunga bao lake la tatu msimu huu na kuipa Arsenal uongozi wa 2-1 baada ya kazi nzuri ya Victor Gyokeres kumruhusu Martin Odegaard kumpasia mchezaji huyo wa zamani wa West Ham United, ambaye alipiga shuti safi kutoka nje kidogo ya boksi.
Kazi nzuri ya Noni Madueke upande wa kulia ilimwona mchezaji huyo wa kimataifa wa England akimpita kwa urahisi Antoine Semenyo, anayetajwa kujiunga na Manchester City, kabla ya kupiga pasi ya chini kuvuka mbele ya lango.
Baada ya mpira kubabatizwa ndani ya boksi, Gabriel alikuwa hapo kuupiga na kuufunga katika nguzo ya pili. Baada ya dakika 65, Arsenal waliweza kuingiza Bukayo Saka, Leandro Trossard na Gabriel Jesus.
Dakika tano baadaye, Odegaard alimpa Saka pasi ya ujanja nyuma ya Adrien Truffet, na winga huyo alimpasia Rice aliyekuwa akiingia ndani ya boksi ili kuongeza bao la tatu. Eli Junior Kroupi alifunga bao la kuvutia kwa shuti la umbali wa mita 25 dakika ya 75, na kuipa Bournemouth matumaini ya kupata sare.
Bournemouth walikuwa na nafasi kadhaa katika mchezo huo, huku Marcus Tavernier na Justin Kluivert wakimsumbua kipa David Raya.
Hata hivyo, juhudi zao nyingi zilitoka nje ya boksi. Hilo lilikuwa moja ya tofauti kuu kati ya timu hizo. Arsenal, kama vinara wa ligi, walionyesha nguvu na kina cha kikosi chao kwa kudhibiti mchezo wakati nguvu za Bournemouth zilipoanza kupungua. Ushindi umeifanya Arsenal sasa kujikita kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi sita mbele ya Aston Villa waliopo kwenye nafasi ya pili.